picha ya mtandao
WAHAMIAJI haramu 64 pamoja na wasafirishaji wawili, wamekamatwa na Jeshi la Polisi mkoani Dodoma katika kizuizi cha Chenene Wilaya ya Chamwino wakisafirishwa kuelekea Afrika Kusini.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Gilles Muroto, alisema jana kuwa wahamiaji hao walikamatwa majira ya asubuhi jana.
Alisema waliwakamata kutokana na kuwa na taarifa juu ya wahamiaji hao siku tatu zilizopita kwamba wametoka katika mpaka wa Tanzania na Kenya, Holili.
Alisema kutokana na taarifa hizo waliweka mtego katika kizuizi hicho ambapo gari ilipofika ilipekuliwa na kukuta wahamiaji hao haramu.
Alibainisha kuwa mbinu waliyotumia waliweka maboksi kusudi gari linapokaguliwa lionekane limebeba maji, lakini ndani yake kuna wahamiaji haramu waliokuwa wamefichwa.
“Mbali na hawa wahamiaji haramu 64, pia tunawashikiria wasafirishaji wao, Alois Mvungi (34) mkazi wa Pasua na msaidizi wake, Emanuel Sambara (39), mkazi wa Majengo mkoani Kilimanjaro,” alisema.
Muroto alisema wasafirishaji hao walikamatwa wakiwa na Sh. Milioni 5.4, “Kwa taarifa tulizonazo wahamiaji hawa walikuwa wakitolewa mpaka wa Holili kupitia mkoani Dodoma hadi Mbeya kwa ajili ya kuelekea Afrika Kusini,” alisema Muroto.
Kufuatia hali hiyo, kamanda huyo alitoa wito kwa wakazi wa Dodoma kwamba suala la uhamiaji haramu sasa ni tatizo sugu na baya, hivyo watoe taarifa wanapowaona.
Mmoja wasafirishaji, Sambara akizungumza huku akiwa chini ya ulinzi akiwa amefungwa kwa pingu, alisema walikodiwa na wahamiaji hao haramu na hawakujua kitakachowatokea.
Akizungumzia tukio hilo, Ofisa Uhamiaji wa Mkoa wa Dodoma, Peter Kundy, alifafanua kuwa Sheria ya Uhamiaji ya Mwaka 2005, inatoa adhabu kwa wahamiaji haramu ni kulipa faini ya Sh. 500,000 ama kifungo cha miezi sita jela.
Alisema kwa upande wa mmiliki wa gari kama mahakama itajiridhisha lilikuwa likitumika kwa ajili ya usafirishaji wa wahamiaji haramu, ni kulitaifisha na wale waliokuwa wakiwasafirisha watalipa faini ya Sh. milioni 20 au kifungo cha miaka 20 jela ama vyote kwa pamoja.
Nipashe ilishuhudia wahamiaji hao wakishushwa kwenye lori namba T756 BMY huku wakiwa wamebeba mikate, na wengine wakilia baada ya kugundua kuwa wamekamatwa, Mmoja wao alionekana kushindwa kutembea, hivyo kubebwa na polisi.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA