Meja Jenerali alikabithi bunge taarifa ya Lugumi.

Mradi wa kuweka mashine za utambuzi wa vidole katika jeshi hilo ulifanywa na Kampuni ya Lugumi.


Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) ya Bunge, Naghenjwa Kaboyoka jana alithibitisha taarifa hiyo ya utekelezaji kukabidhiwa kwa Bunge na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira.

Alisema Katibu Mkuu huyo alifika kwenye kamati ya PAC jana na kutoa taarifa kuhusu kuwasilishwa kwa taarifa ya utekelezaji wa maagizo ya Bunge.

“Baada ya taarifa hiyo kupelekwa Ofisi ya Bunge, Spika Job Ndugai akishaipokea ndiyo ataiwasilisha kwa kamati ya PAC,” alisema Kaboyoka.

Alibainisha baada ya Katibu Mkuu wa Wizara kutoa taarifa kwa kamati juu ya kuwasilishwa kwa taarifa ya utekelezaji wa maagizo ya Bunge, PAC haikujajadili tena taarifa hiyo.

Lugumi ilikuwa inatekeleza mradi wenye thamani ya Sh. bilioni 37 wa kusimika mfumo wa utambuzi wa alama za vidole kwenye vituo vya polisi nchi nzima.

Mwanzoni mwa Aprili, PAC ilieleza kuwa kampuni ya Lugumi ililipwa Sh. bilioni 34 na Jeshi la Polisi mwaka 2011 ili kufunga vifaa hivyo katika vituo 138 vya polisi nchini, lakini ni vituo 14 tu ndivyo vilivyokuwa vimefungiwa, licha ya kulipwa fedha hizo ambazo ni sawa na asilimia 90 ya malipo yote ya kazi hiyo.

Ulipaji wa asilimia 90 ya malipo ya kandarasi kabla ya kukamilika kwa kazi ni kinyume na sheria ya manunuzi ya umma.

Wakati wa kuahirishwa kwa kikao cha bajeti Juni 30, Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson alisema Bunge limeagiza Serikali kuhakikisha mfumo huo unafanya kazi, na pia Kamati ya PAC ifuatilie na kutoa taarifa katika taarifa ya mwaka ya kamati.

Alisema kamati ilibaini kuwa mradi huo unafanya kazi katika vituo 14 pekee kati ya 108 jambo ambalo lilikuwa linaenda kinyume na mkataba.

Aidha, Dk. Tulia alisema kutokana na changamoto hiyo kamati ya PAC ilimtaarifa Spika, ambapo aliwaruhusu kuunda kamati ndogo ambayo nayo ilifanya ukaguzi na kubaini mapungufu.

Naibu Spika alisema baada ya kamati hiyo kuipitia, ilikubaliana kukabidhi taarifa hiyo kwa Spika ambapo na yeye ameona kuwa inastahili kuwasilishwa.

Alisema kwa mujibu wa kanuni Spika ataweka utaratibu wa kujadili taarifa ya kamati endapo kamati yoyote katika utekelezaji wa majukumu yake itaona kuwa kuna mambo ya utekelezaji inaweza kutoa taarifa maalum kwa waziri husika ili aweze kuchukua hatua zinazostahili.

Chapisha Maoni

0 Maoni