SERIKALI: Tuna mambo mengi, siyo mikopo pekee

Serikali imesema kuwa ina mambo mengi ya kushughulikia katika elimu na siyo mikopo ya elimu ya juu pekee, hivyo wanafunzi wanatakiwa kuwa wavumilivu.


Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi Mhandisi Stella Manyanya bungeni Dodoma, wakati akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Kilolo, Mh. Venance Mwamoto aliyetaka kujua hatma ya wanafunzi wa elimu ya juu wanaolalamika kukosa mikopo.

Mhandisi Manyanya amesema kuwa hadi sasa tayari awamu ya kwana ya fedha za mikopo imekwisha toka, na kwamba kilichosababisha ucheleweshwaji ni zoezi la uhakiki wa wanafunzi ili kupata wanafunzi wenye sifa sitahiki.

"Siyo kila muombaji wa mkopo atapata mkopo, mikopo hii itatolewa kwa walengwa pekee ambao ndiyo wahitaji, serikali inashughulikia mambo mengi katika sekta ya elimu na siyo mikopo pekee, kwahiyo pesa nyingine zinatumika kwenye mambo mengine kama vile ujenzi wa mabweni, maabara na miundombinu mingine"

Aidha Mhandisi Manyanya amewahakikishia wanafunzi kuwa tatizo la mikopo litamalizika ndani ya wiki hii huku akisisitiza kuwa mikopo hiyo itakuwa ni kwa walengwa pekee na siyo wanafunzi wote.

Kufuatia suala la mikopo hiyo kuanza kutikisa bunge katika kikao chake cha kwanza hii leo, mwenyekiti wa kikao hicho ameiagiza serikali kuandaa maelezo kuhusu sakata hilo.

Chapisha Maoni

0 Maoni