"Siasa si Mchezo Mchezo" Mnada wa wadaiwa Sugu wa TRA waingiliwa

MNADA wa mali za wadaiwa sugu waliotangazwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Novemba 26, mwaka huu, umeingia doa, baada ya taasisi hiyo kurekebisha orodha ya wadaiwa wake hao iliyowatangaza awali.


Katika orodha hiyo iliyotangazwa kwa mara ya kwanza katika moja ya magazeti ya kila siku nchini sambamba na kupachikwa katika tovuti ya mamlaka hiyo kwa siku kadhaa, Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) inayoongozwa na Salma Kikwete, mke wa Rais wa Awamu ya Nne imeondolewa kwenye orodha husika kwa kile kilichoelezwa ni makosa yaliyofanywa awali na TRA.

Taarifa ya kuondolewa kwa WAMA kwenye orodha hiyo imetolewa na Kamishna Mkuu wa TRA, Alphayo Kidata, Jumatatu jioni wiki hii, ikiwa ni taarifa ya tatu kutolewa na taasisi tatu tofauti nchini kuhusu orodha ya mnada huo, ndani ya siku chache.

Katika toleo lililopita la gazeti hili, Raia Mwema liliandika kuhusu hatari ya kupigwa mnada kwa mali hizo endapo WAMA itakuwa haijalipa kufikia Januari mwakani.

Msingi wa habari hiyo ya gazeti hili ilikuwa ni taarifa ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) iliyoeleza kuwa mali za taasisi hizo hatarini kupigwa mnada kwa vile hazijalipiwa kodi inayotakiwa.

Hata hivyo, mara baada ya kutoka kwa habari hiyo iliyokuja kutawala kwenye vyombo vya habari rasmi na mitandao ya kijamii, ziliibuka taarifa tofauti tatu kutoka katika taasisi tofauti.

Kwanza, ilikuwa ni taarifa kutoka WAMA iliyokana kuwa na deni lolote kuhusiana na mzigo wa vitabu kutoka Japan. Katika maelezo yake yaliyochapwa katika baadhi ya vyombo vya habari, WAMA ilieleza kuwa ilikwishafanya malipo ya mali hizo tangu Julai mwaka huu.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotolewa Desemba 2 mwaka huu, WAMA kupitia kwa Katibu Mtendaji wake, Daudi Nassib, ilikana kuwa na mzigo wowote uliozuiwa na TRA.

“Kwa niaba ya WAMA, napenda kutoa masikitiko yetu kwamba habari hizo ni za uongo na hazina ukweli wowote. Kwa maoni yetu, gazeti lililotoa habari hizo lina dhamira mbaya dhidi ya WAMA na mama Salma Kikwete. Nia yao ni kupaka matope na kuchafua majina na sifa ya taasisi yetu na kiongozi wake, ilieleza taarifa hiyo.

Siku mbili baadaye, Desemba 4 mwaka huu, Ikulu kupitia taarifa rasmi iliyosambazwa na Kurugenzi ya Mawasiliano, ilieleza kusikitishwa kwake na kusambazwa kwa habari hizo ilizosema zinataka kumgombanisha Rais John Magufuli na Rais mstaafu, Jakaya Kikwete.

Pamoja na mambo mengine, taarifa hiyo ilieleza; “Katika siku za karibuni baadhi ya vyombo wa habari na mitandao ya kijamii imechapisha taarifa zinazomhusisha mama Salma Kikwete na taasisi anayoiongoza ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) kwamba imeshindwa kulipia kodi mizigo mikubwa iliyoiingiza nchini na hivyo kuwa hatarini kupigwa mnada.

“Taarifa hizo zimemhusisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli kuwa anahusika kuzuia mizigo hjyo bandarini mpaka hapo itakapolipiwa kodi.

“Tunapenda kuutarifu umma kuwa taarifa hizo si kweli na ni uzushi, na Rais Magufuli hajawahi kuzuia wala kuagiza kuzuiwa kwa mizigo ya Mama Kikwete.

“Rais Magufuli amesikitishwa sana na uzushi huo unaofanywa kwa lengo la kumchafua Rais mstaafu wa Awamu ya Nne Dk. Jakaya Mrisho Kikwete na familia yake na amewataka waandishi wa habari na wombo vya habari nchini kuacha kuandika na kuchapisha taarifa za uzushi na badala yake wazingatie weledi na kufuata sheria”.

Ikimnukuu Magufuli mwenyewe, taarifa hiyo ilisema “Nimesikitishwa sana na uzushi unaofanywa dhidi ya Rais Mstaafu Dk. Jakaya Mrisho Kikwete na mke wake. Tafadhali mnaotengeneza uzushi huu muache mara moja, muacheni rais mstaafu apumzike''.

“Rais Mstaafu Kikwete amefanya makubwa kulitumikia taifa hili, amestaafu na amepumzika. Narudia muacheni apumzike, serikali haiwezi kuendelea kuvumilia uzushi na uchonganishi unaofanywa kwa makusudi kuwachafua viongozi wastaafu'' taarifa hiyo ilimnukuu Magufuli akionya.

Hata hivyo, taarifa hiyo ya Ikulu haikusema pia kwamba taarifa ya TRA iliyotolewa kupitia gazeti rasmi la CCM pia ilikuwa ni ya uzushi na uchonganishi.

Tangazo hilo rasmi la TRA halikuhusu WAMA pekee bali pia taasisi nyingine mbalimbali za kidini na balozi zilitajwa kuwa katika tishio la kupigwa mnada kwa mali zake zilizotajwa.

Katika mazungumzo yake na Raia Mwema kwenye toleo lililopita la gazeti hili, Mkurugenzi wa Elimu kwa Huduma za Walipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo, alikiri kuwapo kwa mizigo ya WAMA inayoweza kupigwa mnada endapo hazitalipwa kufikia tarehe ya mnada.

Hata hivyo, juzi Jumatatu, TRA kupitia kwa Kamishina Mkuu, Alphayo Kidata, ilitoa taarifa rasmi kuhusu sakata hilo na kueleza kwamba orodha iliyoingiza jina la WAMA kama wadaiwa ilikuwa na makosa.

Ingawa taarifa ya TRA inaonyesha kuwa ilifanya makosa kuweka jina la WAMA, kama inavyodai, inaonekana imeamua kutua mzigo wa lawama kwa magazeti na vyombo vya habari vilivyotumia taarifa yao hiyo.

“Tunapenda kutoa ufafanuzi kwamba taarifa zilizoandikwa na baadhi ya magazeti hivi karibuni kwamba vitabu hivyo viko katika orodha ya kupigwa mnada kwa sababu ya kutolipiwa kodi si sahihi. Magazeti husika yalitumia orodha iliyoingiza jina la WAMA kimakosa ili kujenga hoja hiyo potofu, ilieleza taarifa hiyo ya Kidata.

Taarifa hiyo ya TRA ilifafanua kuwa WAMA iliingiza nchini maboksi 11 ya vitabu na kamusi kutoka Japan na kwamba vililipishwa tozo ya jumla ya shilingi 148,921. Vitabu hiyo vilichukuliwa na taasisi hiyo Agosti mwaka huu

Chapisha Maoni

0 Maoni