Wafanyabiashara wauchambua utawala wa JPM

Wadai nchi iko kwenye kipindi cha mpito ambapo haitakuwa ajabu kusikia baadhi ya watu wakilalamika sana kuhusu hali ya maisha.


Wamesema, kwa muda mrefu ilikuwa haijulikani ni nani anayefanya biashara halali na haramu kwa sababu kulikuwa na mfungamano wa biashara halali na haramu. Wametoa mfano, mtu aliyekopa benki na kujenga nyumba lakini anapata wapangaji ambao kipato chao kilikuwa haramu. Kudhibitiwa kwa biashara haramu kunamfanya mpangaji kushindwa kulipa kodi ya upangaji na matokeo yake hata mwenye nyumba anajikuta kwenye tatizo na benki kwa sababu wapangaji wake wameshindwa kulipa kodi.

Mabenki yalikuwa yanatoa mikono kwa watu wasiofaa kupewa mikopo na matokeo yake kwa sasa wameshindwa kulipa huku hali hiyo ikiathiri hata wale ambao wanafaa kupewa mikopo.

Wamedai uchumi uliokuwepo haukuwa endelevu na haunufaishi wananchi wote. Kwa mfano, viwanja kama kigamboni vilikuwa vinauzwa kwa bei ya shilingi milioni 100 kwa sababu kulikuwa na kundi la watu wenye pesa chafu ambao walikuwa wanaziwekeza kwenye ardhi na majengo. Bei hii ya viwanja na nyumba iliwaondoa katika soko wafanyakazi watii wengi serikalini na kwenye mashirika mbali mbali kwa sababu vipato vyao halali haviwawezeshi kununua kiwanja kwa bei hiyo mbaya zaidi hata serikali haikuweza kuongeza vipato vyao kwa sababu haikuwa na pesa za kutosha.

Baadhi yao wamedai, nchi inakoelekea kwa sasa ndio kwenye uchumi halisi wa mtanzania na katika kufanya hivyo kuna wengine wataathirika wakati huu wa mpito hasa ikichukuliwa kuwa asilimia 40 ya pesa za serikali zimeelekezwa kwenye maendeleo na siyo matumizi ofisini.

Anachokifanya Rais Magufuli ndicho kinachofanywa na wafanyabiashara makini. Fikra na shabaha yake ni sawa na wafanyabiashara makini kama vile kuzidisha mapato na kukata matumizi yasiyo ya lazima ambapo faida nzuri hupatikana ili kuwekeza tena kwenye jamii. Mafanikio ya kazi za Rais yataonekana baada ya miaka miwili na kuendelea.

Baadhi yao wamedai tulikuwa kwenye uchumi ambao kwa nje unaonekana mzuri lakini kwa ndani ulikuwa unaelekea shimoni.

Wengine wamewakosoa watendaji wa serikali kwa kutafsiri vibaya ujumbe wa Rais kuhusu vita vya ukwepaji kodi, ufisadi na rushwa kiasi kwamba kwa sasa wanadhani kila mfanyabiashara ni mkwepa kodi. Wanahitaji kuelewa sio kila mfanyabiashara ni mkwepa kodi na kwa maana hiyo, waboreshe huduma za customer service na kuwaona wafanyabiashara ni wadau muhimu wa maendeleo nchini.



Chapisha Maoni

0 Maoni