Huyu ndio Mchezaji wa Kwanza kutupiwa virago vyake Simba


BEKI wa kulia Hamad Juma ameachwa katika klabu ya Simba kutokana na sababu za utovu wa nidhamu, imeelezwa.


Habari za ndani ambazo Bin Zubeiry Sports – Online imezipata zinasema kwamba Hamad alianza kuonyesha tabia zake za utovu wa nidhamu mapema tu baada ya kusajiliwa na kuna wakati zilimsababishai madhara makubwa.

“Kuna wakati ilibidi uongozi useme uongo kwamba mchezaji huyu alianguka chooni, lakini ukweli ni kwamba mambo yake aliyokuwa anayafanya ya utovu wa nidhamu ndiyo yalimsababishia kilichompata,”alisema kiongozi mmoja wa Simba ambaye hakutaka kutajwa jina.

Lakini benchi la ufundi pia chini ya kocha Mcameroon, Joseph Marius Omog nalo lilishindwa kuvumilia tabia za mchezaji huyo na kumripoti kwa uongozi.

Na kuna wakati beki chaguo la kwanza wa kulia, Mkongo Janvier Besala Bokungu alikuwa anatumikia adhabu ya kadi, kocha Omog akalazimika kumpanga kiungo Muzamil Yassin katika nafasi hiyo, badala ya Hamad Juma kwa tabia zake.

Mchezaji huyo alisajiliwa Simba msimu uliopita kutoka Coastal Union ambayo iliteremka Daraja na baada ya msimu mmoja tu wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara anatupiwa virago.    

Chapisha Maoni

0 Maoni