MKAZI wa wilayani Itilima mkoani Simiyu, Matilda Maghembe (16)
amelazwa katika Hospitali Teule ya Mkoa ya Somanda mjini Bariadi, baada
ya kudaiwa kumwagiwa mwilini dawa ya kimiminika aina ya Lysol na muuguzi
katika Zahanati ya Sunzula baada ya kujifungua.
Kutokana na madhara hayo, Matilda, mkazi wa kijiji cha Sunzula amelazwa
katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) katika Hospitali ya Somanda.
Tayari Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy
Mwalimu amemwagiza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Simiyu kufuatilia tukio hilo
la Oktoba 16 mwaka huu, baada ya kupata taarifa na kuona picha kupitia
mitandao ya kijamii.
Chanzo cha hasira za muuguzi huyo ambaye jina lake halijafahamika,
kimetajwa ni kushindwa kuelewana katika malipo na mama wa Matilda,
Hungwa Mahangwa (50) anayedaiwa kuombwa Sh 6,000 na muuguzi, ilhali mama
huyo akiwa na Sh 5,000.
Wakizungumza katika Hospitali ya Wilaya ya Maswa mkoani hapa alikokuwa
amelazwa Matilda kabla ya kuhamishiwa Hospitali ya Somanda, ndugu wa
mgonjwa huyo wamemtuhumu muuguzi wa zahanati hiyo kwa kitendo cha
kinyama alichokifanya.
Walidai Matilda alifika katika zahanati hiyo na kujifungua salama mtoto
wa kiume Oktoba 14, mwaka huu na kutakiwa kurudi siku iliyofuata ili
kutolewa gozi aliyowekewa baada ya kuonekana alikuwa akivuja damu baada
ya kujifungua na kuruhusiwa kurudi nyumbani.
Walidai hawakurudi siku ile waliyoelezwa na hivyo kurudi Oktoba 16,
mwaka huu akiwa amefuatana na mama yake mzazi, jambo ambalo lilionesha
kutomfurahisha muuguzi huyo ambaye alianza kuwatolea lugha chafu ya
matusi.
“Tulielezwa tumrudishe katika zahanati hiyo mgonjwa siku iliyofuata,
lakini tulizidisha siku moja maana tulikosa usafiri sasa tulipofika
alianza kututolea lugha ya matusi,” alisema mama wa Matilda.
Alidai walikubali kumpokea mgonjwa huyo na kuanza kumpatia matibabu
akiwa kitandani ndipo muuguzi huyo alipoomba fedha Sh 6,000, lakini wao
wakawa na Sh 5,000 jambo ambalo lilionekana kutomfurahisha na hivyo
kuingia chumba kimojawapo na kutoka na kopo lililokuwa na dawa hiyo na
kummwagia mwilini mgonjwa huyo aliyelia kwa uchungu na hatimaye kupoteza
fahamu.
Alisema baadaye bintiye alizinduka, lakini alikuwa akilia kutokana na
maumivu baada ya kuungua vibaya sehemu mbalimbali za mwili wake zikiwemo
makalio, mapaja na sehemu za siri na hivyo muuguzi huyo kuwashauri
wampeleke katika Hospitali ya Wilaya ya Maswa kwa matibabu zaidi kwa
madai kuwa ameishiwa maji.
Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dk Luguga Vedastus alikiri
kumpokea mgonjwa huyo tangu Oktoba 21, mwaka huu na hivyo kabla ya rufaa
alitaka ajiridhishe kwa kupata taarifa zaidi kutoka kwa mwenzake wa
Itilima, lakini wakati akiendelea na mawasiliano, alipigiwa simu kutoka
wizarani wakitaka kufahamu kwa undani suala hilo.
Akizungumzia sakata hilo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dk Magenda
Kihulya alikiri tukio hilo na kueleza dawa aliyomwagiwa inatumika
kusafishia sakafu ili kuua wadudu wanaoeneza magonjwa ya kuambukiza kama
kipindupindu na haifai kwenye mwili wa binadamu, kwani ni kali kama
tindikali.
“Ni kweli tukio lipo na mgonjwa tunaye hapa hata sisi hatukuwa na
taarifa hizi tumepigiwa simu toka wizarani hivyo tunachokifanya
tunaondoka na mgonjwa hadi mjini Bariadi kwa matibabu zaidi huku
tukiendelea kutafuta muuguzi aliyefanya kitendo hiki,” alisema.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA