KIGOMA: Zaidi ya abiria 50 wanusurika kifo baada ya basi kutumbukia katika mto Malagarasi

Zaidi ya abiria 50 waliokuwa wakisafiri kutoka vijiji vya mwambao wa kusini katika ziwa Tanganyika tarafa ya Buhingu wilayani Uvinza mkoani Kigoma wamenusurika kufa baada ya basi aina ya Saratoga walilokuwa wakisafiria kuelekea mjini Kigoma kutumbukia katika mto Malagarasi wakati basi hilo na abiria wengine wakivushwa katika kivuko cha mto huo.


Mashuhuda wa tukio hilo pamoja na nahodha wa kivuko cha MV Malagarasi wamesema basi hilo lenye namba za usajili T 938 AGQ limetumbukia mtoni baada ya kivuko kutia nanga upande wa pili baada ya kurudi nyuma taratibu huku abiria wote wakiwa wameshuka na kwamba hilo ni tukio la tano kutokea katika eneo hilo hivyo wameiomba serikali kujenga daraja ili kuepusha maafa yanayoweza kutokea.

Akizungumza katika eneo la tukio, kamanda wa polisi mkoa wa Kigoma kamishna msaidizi mwandamizi wa polisi Ferdinand Mtui amesema katika ajali hiyo hakuna mtu aliyepoteza maisha na kwamba jitihada zinazofanywa sasa ni wazamiaji kujaribu kulitoa majini basi hilo.    

Chapisha Maoni

0 Maoni