HATIMAYE agizo lililotolewa na Rais Dk. John Magufuli la ‘kufyeka’
mishahara ya vigogo wa Serikali, wakiwamo wa mashirika ya umma waliokuwa
wakilipwa hadi Sh milioni 40 kwa mwezi, limeanza kutekelezwa.
Akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam juzi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki,
alisema tayari kazi ya ‘kufyeka’ mishahara hiyo imetekelezwa tangu
mishahara ya Julai, mwaka huu.
Hatua hiyo, imekuja baada ya Rais Magufuli kuagiza kushushwa kwa viwango
vya mishahara ya viongozi wa mashirika ya umma, ambao baadhi yao
walikuwa wakilipwa Sh milioni 36 hadi 40 kwa mwezi.
“Tayari kazi ya kupunguza mishahara mikubwa ya watumishi wa umma
imeshatekelezwa tangu malipo ya Julai, hakuna mtumishi yeyote wa umma
anayelipwa zaidi ya Sh milioni 15,” alisema Waziri Kairuki.
Machi 30, mwaka huu akiwa wilayani Chato, Rais Magufuli alisema kuna
watumishi wa umma ambao wanalipwa kiwango kikubwa cha mishahara na
kujikuta wakiishi maisha kama malaika, hivyo ni lazima ishushwe ili
waishi kama shetani.
Hatua ya Rais Magufuli, kupitisha ‘panga’ na kuweka uwiano wa mishahara
kwa watendaji wa taasisi hizo, inaelezwa kuwa itasaidia kuwapo
uwajibikaji na usawa.
Rais Magufuli alisema kuwa ameunda timu ya wataalamu ambayo inafanya
kazi ya kupunguza mishahara hiyo na kufikia Sh milioni 15 kwa mwezi ili
asipatikane Mtanzania anayelipwa zaidi ya kiwango hicho.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA