Wadau salamu!
Makala yangu ya leo ni kujaribu kuangalia ufanisi na uhalisia wa mambo yanayoendelea chini ya mwavuli wa mada yangu tajwa hapo juu, naomba kidogo mniazime masikio na endapo sijafikia kufikiria kama ulivyotarajia, basi nami ni binadamu, jaza mapungufu yangu.
Serikali ya awamu ya tano chini ya Dkt. JPM imefanikiwa, kwa madai yake, kukusanya kodi kwa takribani 1.3 kila mwezi, na tumeona kuwa serikali imekuwa ikihimiza kulipa kodi kwa makampuni mbalimbali, huku mengine ambayo yameshindwa kulipa kodi hiyo yamekuwa yakichukuliwa naamuzi magumu sana (mfano kampuni ya Mohamed Trans ya Shinyanga, ambayo kwa kushindwa kulipa kodi, ijumaa ya tarehe nne itapigwa mnada) ili tu kurejesha nidhamu ya ulipaji kodi.
Bandarini nako, watumishi mbalimbali wametumbuliwa kwa kuikosesha mapato serikali, na tena utumbuaji wake ni ule wa wazi na kila mwananchi anashuhudia; nadhani hii ni kuwapa imani wananchi kwa serikali yao, n.k.
Wafanyakazi hewa pia tumeona wametumbuliwa na uhakiki bado unaendelea hasa katika uhalisia wa vyeti vya kitaaluma; zoezi ambalo limedumu kwa takribani miezi kadhaa sasa ili kujiridhisha kwa uhalali wa watumishi kuwepo katika kada wanazozitumikia.
Sanjari na hayo, serikali imekuwa ikibana matumizi kwa kupunguza matumizi yasiyokuwa ya lazima. Sote tutakuwa tunakumbuka kuwa, baada tu ya kuapishwa, Mhe. aliziba mianya ya upotezaji fedha za, alivyodai, kodi za walala hoi kwa mbio za mwenge na sherehe za uhuru, kwa hiyo sherehe hizo hazikufanyika. Kilichokuja kutangazwa, kama kumbukumbu yangu haijaenda mlama, ni kwamba, fedha hizo zitaenda kujenga barabara mwanza.
Labda kabla sijaenda mbali kudadafua nini nachotaka kukizungumza, nirejee maelezo ya sheikh fulani aliyekuwa akihojiwa na shirika la utangazaji la TBC FM katika kipindi cha fainali uzeeni, huyu mzee alisema, enzi za utawala wa waingereza, kodi iliyokuwa ikikusanywa kwa wananchi ilikuwa shilingi 12 kwa mwaka. Ijapokuwa wananchi wengi pia walikuwa wanakwepa kuilipa, lakini kodi hiyo ilifanya mambo mengi sana, ilitoa huduma za afya bure na elimu bure kabisa.
Tujiulize tu kwa pamoja, pasi na ushabiki wowote, kama kodi ya shilingi 12 iliweza kutoa huduma zote hizi, je kwa nini trilion 1.3 imeshindwa kufanya hivi? Labda wengi kidogo hawajanielewa nasema nini. Ninachokimaanisha ni hiki. Nenda hospitali za serikali ili ujionee mziki wa gharama ulioko kule, kisha ukija kusoma hapa, basi nadhani utakuwa umenielewa vema. Usikomee hospitalini tu, nenda mashuleni uone hali halisi ya mazingira wanamosomea wanafunzi, licha ya kuwa serikali inasema inatoa elimu bure, nafikiri hali hiyo haitakuficha chochote kiasi kwamba usinielewe nikisemacho. Baada ya hapo, nenda kwa taasisi za elimu za juu, ongea na wanafunzi wa elimu ya juu uwasikilize kinachowakuta kwenye suala la fedha, mizengwe haiishi kwa mwaka mzima sasa, hadi ilifikia hatua fedha za mazoezi ya vitendo ikatolewa nusu.
HIVI, PESA HII YOTE INAYOKUSANYWA KUTOKANA NA KODI, UBANAJI WA MATUMIZI NA UTUMBUAJI WA WAFANYA KAZI HEWA, NI KWA MANUFAA YA NANI?
Maisha mtaani yanazidi kuwa magumu, gharama za maisha zinazidi kupanda, badala ya kushuka kama wengi tulivyokuwa tukitegemea, binafsi hadi kufikia hatua ya kuandika makala hii, sijaelewa tunaelekea wapi, labda nawe msomaji wangu unisaidie kujibu swali hilo hapo juu.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA