CHAMA cha Wananchi – CUF tayari kimemteua mwanachama wake Abdulrazak Khatib Ramadhan kugombea nafasi ya ubunge katika uchaguzi mdogo Jimbo la Dimani Zanzibar, anaandika Pendo Omary.
Nassor Ahmed Mazrui, Naibu Katibu Mkuu wa CUF – Zanzibar ameuambia mtandao wa MwanaHALISI Online kuwa tayari Baraza Kuu la CUF limemteua Ramadhan kuwania nafasi ya ubunge Jimbo la Dimani.
“Jumapili mgombea tuliyempitisha alichukua fomu ya uteuzi kwenye ofisi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Wilaya ya Magharib B,” amesema Mazrui.
Mazrui amesema katika msafara wa kuchukua fomu Ramadhan alisindikizwa na viongozi, wanachama na mashabiki wa CUF.
Katika kinyang’anyiro cha uchaguzi huo mdogo, Chama cha Mapinduzi (CCM), kimemteua Juma Ali Juma kuwa mgombea wake ambapo tayari amechukua fomu katika ofisi za muda za NEC zilizopo Shule ya Sekondari Kiembe Samaki.
Mbali na uchaguzi mdogo wa ubunge atika jimbo la Dimani pia NEC itaendesha uchaguzi wa udiwani katika kata 22 hapa nchini ambapo jumla ya Sh. 3 bilioni zitatumika.
Ramadhan Kailima, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC amesema maandalizi ya chaguzi hizo zote yamekamilika, ambapo Sh. 1.7 bilioni zitatumika katika uchaguzi mdogo Jimbo la Dimani na Sh. 2.2 Bilioni zitatumika kwa ajili ya uchaguzi wa Udiwani katika Kata 22.
Fomu za kugombea zilianza kutolewa tarehe 15 Desemba mwaka huu, ambapo mwisho itakuwa ni tarehe 22 Desemba na Kampeni zitaanza rasmi tarehe 23 Desemba mwaka huu hadi tarehe 21 Januari mwakani.
Uchaguzi mdogo wa Jimbo la Dimani unafanyika kufuatia kifo cha Hafidh Ali Twahir aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo kabla ya kufariki i dunia tarehe 11 Novemba mwaka huu katika Hospitali ya Rufaa Mkoani Dodoma.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA