Prof. Kitila amvaa rais Magufuli, asema aache kudharau tafiti za kitaalamu

PROFESA Kitila Mkumbo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mchambuzi wa masuala ya kisiasa amelaani kitendo cha Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli kutoheshimu tafiti zinazofanywa na wataalamu, anaandika Wolfram Mwalongo.


Prof. Kitila amesema kuwa kitendo cha Rais Magufuli kutengua uteuzi wa Dk. Mwele Malecela aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), ni shambulizi kubwa dhidi ya shughuli za kitaaluma.

Akizungumza leo katika kipindi cha Tuongee Asubuhi ambacho hurushwa na kituo cha runinga cha Star TV, Prof. Kitila amesema “Dk. Mwele hakutangaza kuwepo kwa mlipuko ugonjwa wa Zika hapa nchini bali alitoa matokeo ya utafiti, na siku zote utafiti hupingwa kwa utafiti.”

Prof. Kitila ameshangazwa na taarifa iliyotolewa na Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya aliyekanusha taarifa za utafiti huo. Amesema waziri huyo alipaswa afanye utafiti mwingine unaopingana na ule wa NIMR uliotoa taarifa za kuwepo kwa ugonjwa wa Zika hapa nchini.

“Tafiti zote duniani husomwa na waliofanya utafiti. Utafiti huu ulihusisha wataalamu, vifaa na fedha, sasa iweje serikali itishe wataalam?

“Tumepuuza makabrasha yote ya utafiti kwa tamko la kisiasa lenye nusu ukurasa lililotolewa na waziri. Inaonekana serikali inaogopa kupoteza watalii zaidi kuliko kupoteza wananchi kwa ugonjwa,” amesema Prof. Kitila.

Usiku wa tarehe 16 Desemba, 2016 Rais Magufuli alitangaza kumng’oa Dk. Mwele katika nafasi ya Mkurugenzi mkuu wa NIMR ikiwa ni masaa machache tangu atangaze matokeo ya utafiti uliofanywa na taasisi hiyo na kubaini kuwepo kwa mlipuko wa ugonjwa wa Zika hapa nchini.

Chapisha Maoni

0 Maoni