Mkuu wa chuo mstaafu apandishwa kizimbani

Dodoma. Aliyekuwa Mkuu wa Chuo cha Serikali za Mitaa cha Hombolo(LGTI), Emanuel Gibali na wenzake wawili wamepandishwa kizimbani  Mahakama ya Wilaya ya Dodoma kwa kosa la kupokea rushwa ya Sh 12.4 milioni  kutoka Manispaa ya Morogoro.


Akisoma mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Godfrey Pius, Mwendesha Mashtaka kutoka Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (Takukuru), Biswaro Biswaro  alisema washtakiwa hao  wanakabiliwa na makosa manne ambayo waliyafanya Septemba, 2015 chuoni hapo.

Biswaro aliwataja washtakiwa wengine kuwa ni pamoja na Mkuu wa  Idara ya Utafiti ,Ushauri na Mafunzo Mafupi, Benjamen Magori na Mhasibu wa Chuo hicho, Eliakundi Samanya.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, Hakimu Pius alisema dhamana zipo wazi na kutoa masharti kuwa kila mmoja anatakiwa kujidhamini mwenyewe kwa mali isiyohamishika yenye thamani ya zaidi ya Sh 2 milioni na dhamini moja mwenye barua ya utambulisho kutoka serikali za mitaa.

Watuhumiwa wote  watatu wapo nje kwa dhamana baada ya kutimiza msharti ya dhamana na kesi yao itatajwa tena januari 18, waka 2017 .

Chapisha Maoni

0 Maoni