Kamanda wa Polisi Mkoa wa kilimanjaro, Wilbrod Mutafungwa
Katika tukio hilo, watu wasiojulikana wamemuua mtu mmoja kisha kumtia kwenye kiroba na kukishona kisha kujaribu kuichoma maiti hiyo baada ya kuimwagia petroli.
Tukio hilo jipya lililotokea karibu na Kijiji cha Ongoma, Uru Wilaya ya Moshi, limeibua maswali juu ya aina hii ya mauaji.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala, Salum Hamduni alisema hiyo ni aina mpya ya mauaji ambayo mpaka sasa jeshi hilo linaendelea kuyachunguza.
“Kwa kweli hii ni aina mpya haikuwapo na ndiyo maana polisi wanaendelea kufanya uchunguzi kujua yanasababishwa na nini na kwa nini wauaji wanafanya hivyo,” alisema.
Lakini Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Wilbrod Mutafungwa alisema anaendelea na uchunguzi kujua aina hiyo ya mauaji katika mkoa wake tu, “Siwezi kuzungumzia hili suala kwa ujumla, hata wewe usilijumuishe ukasema ni aina ya mauaji yanayofanana. Ila kwa mkoa wangu tunaendelea kufanya uchunguzi.”
Baada ya kubainika kwa maiti saba katika Mto Ruvu, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba akikaririwa akisema kwamba huenda walikuwa ni wahamiaji haramu huku Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiagiza kufanyika uchunguzi.
Wakati Waziri Mkuu akiagiza uchunguzi, wananchi wa maeneo ilikoopolewa miili hiyo saba katika Mto Ruvu, walisema kwamba wamekuwa wakiona matukio mengi ya aina hiyo.
Walisema mtindo huo wa utupaji miili inafanana kwa kuwa huwekwa katika mifuko hiyo, kushonwa kwa manila na kutumbukizwa mtoni ikiwekewa mawe ili izame.
Tukio la Moshi
Katika Kijiji cha Ongoma, watu ambao hawajajulikana waliokuwa na gari dogo wanadaiwa kumuua mtu huyo na kishamuweka kwenye kiroba na kuuchoma mwili wake kwa petroli.
Kabla ya kumchoma moto, watu hao wanaodaiwa kuwa walikuwa wawili, wanunua lita tano za petroli eneo la Timbirini na kisha kuzunguka eneo la Mamba na gari lao hadi jirani na Ongoma. “Hakuna mtu aliyejua kama hilo gari lilikuwa na maiti au hao watu wana nia ovu mpaka tulipoona moshi unafuka eneo walilomchomea, tulipofika ndipo tukaona ni mtu,” alisema mmoja wa mashuhuda ambaye hakutaka kutajwa jina.
Awali, ilidaiwa kwamba marehemu alikuwa amevaa nguo zinazofanana na za wafungwa jambo ambalo Kamanda Mutafungwa alilikanusha akisema hana taarifa za jambo hilo na halina ukweli wowote.
“Tumeuchukua mwili kwa ajili ya uchunguzi na bahati mbaya sana hadi sasa haujatambuliwa kuwa ni nani,” alisema Kamanda.
Hata hivyo, alisema Polisi inawashikilia watu kadhaa ambao hakutaja idadi yao kwa mahojiano juu ya tukio hilo.
Aliwaomba wananchi wenye taarifa sahihi ikiwamo watu waliohusika na gari lililotumika ili zisaidie kuwanasa watu waliofanya unyama huo.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA