Dodoma watisha, washusha wakali toka Cameroon


CHAMA cha soka mkoani Dodoma (DOREFA) kikishirikiana na Uongozi wa timu ya Polisi kimeandaa mechi ya kirafiki ya kimataifa kati ya Polisi Dodoma dhidi ya RC Bafoussam ya Cameroon itakayofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri saa 10 jioni Jumapili ya sikukuu ya Krismas.



Mchezo huo utakuwa kipimo kizuri kwa Polisi inayoshiriki ligi daraja la kwanza ambapo mkoa huo unafanya jitihada kubwa ya kuirejesha ligi baada ya kukosekana kwa muda mrefu.

Mwenyekiti wa DOREFA Mulami Ng'ambi ameiambiaBOIPLUS kuwa mchezo huo utahamasisha wakazi wa mkoa huo kupenda soka ili jitihada zinazofanywa na chama hicho za kuwa na timu inayoshiriki ligi kuu zizae matunda.

Ng'ambi pia alisema lengo jingine la mchezo huo ni kuendeleza mpira kwa  kushirikiana na Bafoussam kwa kuanzisha Akademi ya Soka mkoani humo kwa ajili ya kukuza vipaji ambavyo vitakuwa msaada katika siku za baadae.




Tayari timu hiyo inayoshiriki ligi kuu nchini Cameroon ina kituo cha kukuza vipaji Kenya na ndiyo wamewauzia Azam FC baadhi ya  wachezaji  kwenye dirisha dogo la usajili lililopita.

"Tunawaomba wapenzi wa soka mkoani Dodoma wajitokeze kwa wingi na tumeweka viingilio vya chini katika sikukuu ya Krismas ili kila mtu aweze kuhudhuria," alisema Ng'ambi.

Kwa muda mrefu mkoa wa Dodoma umeshindwa kupata timu inayoshiriki ligi kuu Tanzania bara na jitihada zinafanyika kuhakikisha wanapata mwakilishi hasa kipindi hiki ambacho Serikali yote ya awamu ya tano inahamia mkoani humo.

Viingilio katika mchezo huo vitakuwa ni shilingi 5,000 kwa VIP na 3000 kwa mzunguko ili iwe rahisi kwa wadau wengi wa soka waweze kujitokeza.

Chapisha Maoni

0 Maoni