Mamlaka za maji zatakiwa kuzalisha maji ya kutosha kuhudumia viwanda


kaimu
Kaimu katibu Mtendaji Wizara ya Fedha na Mipango kwa upande wa Tume ya Mipango Bibi Flotrence Mwanri akielekea katika ukaguzi wa mradi wa uboreshaji huduma za maji safi na usafi wa mazingira mjini Lindi. Kulia (mwenye t-shirt) ni Meneja wa Mamlaka ya Maji Lindi, Mhandisi Idris Sengulo, pembeni yake ni Mhandisi Mshauri wa Mradi huo, Francis Fumbuka na upande wa kushoto ni Mkandarasi wa mradi huo Bw. Rajendra Kumar.

kaimu-1
Kaimu katibu Mtendaji Wizara ya Fedha na Mipango kwa upande wa Tume ya Mipango Bibi Flotrence Mwanri akiangalia mitambo ya Maji safi Mjini mtwara. Pembeni yake ni Mkurugenzi Mamlaka ya Maji Mtwara Mjini, Mhandisi Mashaka Sitta.
kaimu-2
Mkandarasi wa mradi mradi wa uboreshaji huduma za maji safi na usafi wa mazingira mjini Lindi, Bw. Rajendra Kumar akitoa maelezo  mbele ya Kaimu Katibu Mtendaji anayeongoza timu ya wataalamu wa Ukagauzi wa miradi kutoka Tume ya Mipango.
kaimu-mae
Mkurugenzi Mamlaka ya Maji Mtwara Mjini, Mhandisi Mashaka Sitta akitoa maelezo kwa timu ya wataalamu wa kutoka Tume ya mipango  juu ya namna wanavyotibu maji safi kabla ya kuyasambaza kwa wananchi.
kaimu-ujez
Ujenzi unaoendelea wa mitambo ya maji katika mradi mradi wa uboreshaji huduma za maji safi na usafi wa mazingira mjini Lindi. PICHA ZOTE NA ADILI MHINA, TUME YA MIPANGO
Na Adili Mhina.
Mamlaka za maji nchini zimeshauriwa kuwa na mikakati ya kuboresha na kujenga  miundombinu ya maji inakayokidhi mahitaji ya viwanda na kuachana na mawazo ya  kuzalisha maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani pekee ili kutekeleza malengo ya mpango wa maendeleo wa miaka mitano unaosisitiza uchumi wa viwanda.
Ushauri huo umetolewa kwa nyakati tofauti na Kaimu Katibu Mtendaji  Wizara ya Fedha na Mipango kwa upande wa Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri kwenye ziara yake inayoendelea katika mikoa ya Pwani, Lindi na Mtwara kwa lengo la kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali na ile ya sekta binafsi.
Mwanri alionesha kutoridhishwa na hali ya upatikanaji wa maji kwa ajili ya viwanda baada ya kukagua mradi wa maji wa Kilwa Masoko kwa kutumia chanzo cha mto Mavuji ambao utaanza baada ya kusainiwa kwa makubaliano kati ya Serikali Tanzania na Ubelgiji, ujenzi wa mradi wa uboreshaji huduma za maji safi na usafi wa mazingira mjini Lindi unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania, Ujermani na umoja wa Ulaya pamoja na mradi wa maji safi mjini Mtwara ambapo alibaini kuwa miradi yote imelenga kukidhi mahitaji ya nyumbani pekee bila kuwepo mkakati madhubuti wa kupata maji ya kuhudumia viwanda.
Alieleza kuwa zoezi la kuhamasisha uwekezaji na ujenzi wa viwanda linaloendelea kutekelezwa na viongozi katika ngazi mbalimbali limekuwa na manufaa makubwa kutokana na kujitokeza kwa wawekezaji wanaojenga viwanda katika maeneo mbalimbali ya nchi. Hivyo halmashauri husika zina wajibu kuhakikisha kuwa kuna mazingira rafiki kwa ajili ya uwekezaji ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa maji kwa ajili ya kuhudumia viwanda kwani sio kila muwekezaji atajitafutia maji ya kuhudumia kiwanda chake.
“Mkakati wetu kama taifa ni kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi ya viwanda, tunashukuru kuwa hilo mmelipokea na kulifanyia kazi. Changamoto ninayoiona hapa ni kuwa katika suala la kujenga na kuboresha miundombinu ya maji mmelenga kukidhi mahitaji ya nyumbani peke yake na mmesahau kuwa viwanda navyo vinahitaji maji katika kujiendesha”, alisema Mwanri alipokuwa akikagua mradi wa maji mjini Lindi.
Alisisitiza kuwa serikali ya sasa imelenga katika kupunguza matumizi yasiyokuwa ya lazima ili kuboresha maisha ya wananchi hivyo katika miradi ambayo inatarajiwa kuanza ni vyema kuwa na mawazo ya kujenga miundo mbinu itakayokidhi mahitaji ya maji majumbani na viwandani kwa wakati mmoja badala ya kusubiri viwanda vijengwe ndipo serikali iingie tena gharama ya kupanua au kujenga miundombinu upya ili kukidhi mahitahi hayo.
“Kuanza upanuzi wa miundombinu ili kukidhi mahitaji ya viwanda ni gharama sana na tungeweza kuepuka gharama hizi kama tuamua kuweka miundo mbinu inayoweza kukidhi mahitaji yote hata kama viwanda bado havijajengwa” Alisisitiza.
Mwanri alieleza kuwa ujenzi wa viwanda ni suala mtambuka kwa kuwa linagusa sekta mbalimbali kutoka maandalizi hadi utekelezwaji wake hivyo ni lazima kila mamlaka inayohusika kuhakikisha inatekeleza wajibu wake kikamilifu ili isiwe kikwazo katika maendeleo ya viwanda nchini.
“Tukizungumzia kujenga viwanda sio kwamba wizara ya  viwanda na biashara ndiyo inafanya kila kitu hapana, hili ni suala mtambuka ambalo sekta zingine kama ardhi, mazingira, umeme, maji, barabara na reli, nk, zina nafasi kubwa katika kuhakikisha viwanda vinakuwa katika mazingira salama” alieleza Mwanri

Chapisha Maoni

0 Maoni