POLISI mkoani Tanga limemtia nguvuni na kumfukuza kazi askari wake, Konstebo Maiko Komba aliyekuwa ametoroka kituo cha kazi kwa siku takriban 20, baada ya kuhusishwa na mauaji ya mpenzi wake ambaye naye alikuwa askari mkoani humo.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, David Mnyambugha amebainisha hayo wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari ofisini kwake jana.
Mnyambugha alisema Komba alitoroka kazini Novemba 13, mwaka huu baada ya kudaiwa kumpiga hadi kumsababishia kifo mzazi mwenzake ambaye pia ni askari aliyekuwa na namba WP 9504, Elizabeth Stefano katika tukio lililofanyika jijini Tanga.
“Baada ya Polisi Tanga kupata taarifa za chanzo cha tukio la kifo cha WP Elizabeth kwamba ni ugomvi wa kimapenzi uliokuwa ukiendelea kati yake na mzazi mwenzie huyo PC Komba tayari alikuwa amekimbilia kusikojulikana hivyo hatukufanikiwa kumpata,” alieleza Kaimu Kamanda.
Kamanda Mnyambugha alisema baadaye Jeshi la Polisi Tanga liliendelea kufanya uchunguzi ili kufuatilia askari huyo na hatimaye kupitia taarifa za wasamaria wema ilibainika kwamba Komba alikuwa amejificha jijini Dar es Salaam.
“Juzi Desemba 3, mwaka huu saa sita mchana huko Kiwalani Minazi Mirefu jijini Dar es Salaam askari wetu wa upelelezi wa hapa Tanga kwa kushirikiana na waliopo huko walifanikiwa kumkamata Komba na kumrejesha jijiji hapa akiwa chini ya ulinzi na mpaka sasa bado tunaendelea kumhoji,” alisema Kamanda Mnyambugha na kuongeza:
“Kwa sasa Jeshi la Polisi Tanga limemfukuza kazi kutokana na kosa la utoro kazini ...kuhusu tuhuma za kosa la mauaji bado upelelezi dhidi yake unaendelezwa na huenda atafikishwa mahakamani mara baada ya uchunguzi kukamilika.”
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA