Limemuunga, Rais Magufuli kwa kuweka wazi katika hotuba yake kwamba Serikali ya awamu ya tano itaendelea kuchukua hatua kali ikiwa ni pamoja na kuwatumbua hadharani wale waliozoea kutumbua hadharani mali za Watanzania na pia kuendelea kuchukua hatua kali katika masuala ya rushwa na ufisadi, kwa sababu rushwa ni saratani.
Shirikisho hilo, pia limemuunga Rais kwa tamko lake la hivi karibuni la kuamuru machinga, wachimbaji wadogo na wafugaji kutofukuzwa hovyo hadi mamlaka zinazohusika zitakapotenga maeneo maalumu, likisema pongezi hizo ni kwa sababu Rais amedhihirisha kuwa anajali zaidi masikini na wanyonge.
Salam hizo zimesemwa leo, Desemba 10, 2016, na Katibu Msaidizi wa CCM, Daniel Zenda alipozungumza na Waandishi wa habari Ofisini kwake, Makao Makuu ya Shirikisho la Vyuo vya Elimu ya Juu-CCM, jijini Dar es Salaam, akitoa taarifa ya Shirikisho hilo kuingiza wanachama wapya 100 toka Chuo Kikuu cha Tiba na Afya Muhimbili.
"Kwa kweli tunayo mengi ya kumuunga mkono na kumpongeza Rais, hata hili la kununua ndege sita. Ndege hizi licha ya kusaidia kurahisisha usafiri wa anga pia zitasaidia sana kukuza utalii ambao utachangia kuongeza mapato ya nchi, na ni matarajio yetu mapato yakiongezeka uchumi utakua na hata bei za bidhaa zitapungua na hivyo Watanzania walio wengi kupata nafuu ya maisha".
"Pia sisi kama Watanzania lazima tumuunge mkono na kumpongeza Rais kwa kuendelea kuonyesha dhamira ya serikali ya awamu ya tano kutoa elimu bure kwa kitendo chake cha kutenga kila mwezi sh. bilioni 18.777 kwa ajili ya kutoa elimu bure kwa shule za msingi na sekondari na kwa Vyuo Vikuu sh. Bilioni 483 kutoka sh. bilioni 340 za mwaka jana, hali ambayo imewezesha ongezeko la wanafunzi kutoka 98,000 hadi kufikia 125,000 waliojiunga na vyuo vikuu mwaka huu", alisema Zenda.
Akizungumzia wanachama hao wapya ambao ni madaktari waatarajiwa, katika hafla iliyofanyika Upanga , Dar es Salaam, Zenda alisema, wakati akiwapokea, aliwaambia wamefanya vizuri kujiunga na CCM kwa kuwa wamejiunga na chama makini chenye serikali sikivu inayowajali wanyonge chini ya Rais Dk. John Magufuli.
Shirikisho linawa taka wanafunzi hao na Watanzania kwa kujumla kubeza propaganda zinazosemwa na baadhi ya wanasiasa, kwamba kwa nini ndege zinanunuliwa wakati hakuna dawa katika hospitali.
"Propaganda hii ni upotoshaji mkubwa wenye lengo la kutaka kuwafanya Watanzania hawana akili, maana kila mmoja anajua kwamba katika kipindi hiki kifupi alichoingia madarakani Rais Dk. Magufuli ameboresha sekta ya afya katika maeneo mengi ikiwemo upatikanaji wa dawa katika hospitali, zahanati na vutuo vya afya", Alisema Zenda.
Alisema, miongoni mwa maboresho aliyofanya Rais kwenye sekta ya afya ni pamoja na kuongeza bajeti ya sekta hiyo ya afya kwa ajili ya manunuzi ya dawa kutoka Sh. bilioni 31 hadi kufikia sh. bilioni 250 mwaka huu.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA