Makamu wa Rais wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA), Bi. Noriko Suzuki (kulia), akisikiliza kwa makini maelezo yaliyokuwa yanatolewa na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb) (hayupo Pichani), alipomtembelea na kufanya mazungumzo naye Ofisini kwake Jijini Dar es salaam. Katikati ni Mwakilishi Mkuu Mkazi wa JICA nchini Tanzania, Bw. Toshio Nagase na kulia ni Afisa wa Shirika hilo anayeshughulikia masuala ya usafiri na usafirishaji Bi. Lilian Masalu.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb) (wa pili kulia), akisisitiza jambo wakati alipokuwa akizungumzia umuhimu wa Nishati ya umeme katika kuchochea maendeleo ya viwanda nchini, wakati alipokutana na Makamu wa Rais wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) Bi. Noriko Suzuki, Makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini dar es salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb) (kulia), akizungumzia namna Serikali ya Tanzania ilivyojipanga kutekeleza miradi mbalimbali ya kipaumbele ikiwemo ujenzi wa viwanda mbele ya Makamu wa Rais wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA) Bi. Noriko Suzuki (hayupo pichani), alipomtembelea na kufanya naye mazungumzo ofisini kwake Jijini Dar es salaam. Kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Sheria Bw. Elias Kalist, na kulia kwake ni Mchumi Mkuu, Yosephe Tamamu, wote kutoka Wizara ya Fedha na Mipango.
Mchumi Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Yosephe Tamamu (kushoto), akifafanua jambo katika kikao kati ya Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb) na Makamu wa Rais wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) Bi. Noriko Suzuki. Aliyekaa kulia ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Sheria wa Wizara hiyo Bw. Elias Kalist.
Makamu wa Rais wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) Bi. Noriko Suzuki, akizungumza katika kikao na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb) (hayupo pichani), kuhusu ushirikiano wa kimaendeleo kati ya Tanzania na Japan, Makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb), akimsindikiza mgeni wake, Makamu wa Rais wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) Bi. Noriko Suzuki, baada ya kufanya mazungumzo namna pande hizo mbili zitakavyoimarisha ushirikiano uliodumu muda mrefu katika Nyanja mbalimbali za kiuchumi na kijamii.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb), (kulia) akifurahia jambo na mgeni wake, Makamu wa Rais wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) Bi. Noriko Suzuki, kabla ya kuondoka baada ya kufanya mazungumzo namna pande hizo mbili zitakavyoimarisha ushirikiano uliodumu muda mrefu katika Nyanja mbalimbali za kiuchumi na kijamii. Kulia ni Mwakilishi Mkuu mkazi wa JICA hapa nchini, Toshio Nagase. (Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano-WFM)
Benny Mwaipaja, WFM, Dar es salaam Makamu wa Rais wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA), Bi. Noriko Suzuki, amesema kuwa nchi yake itaendelea kuisaidia Tanzania katika Nyanja mbalimbali za kiuchumi na kijamii ili iweze kufikia malengo yake ya kuondokana na umasikini.
Suzuki ametoa ahadi hiyo baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, ofisini Kwake Jijini Dar salaam. Makamu huyo wa Rais wa JICA, amesema kuwa nchi yake inatumia zaidi ya dola za Marekani Milioni mia moja kila mwaka kusaidia shughuli mbalimbali za maendeleo hapa nchini katika sekta za miundombinu ya barabara, maji, nishati, afya na kilimo.
Miongoni mwa miradi mikubwa inayofadhiliwa na serikali hiyo ya Japan ni barabara ya juu ya mzunguko inayojengwa katika makutano ya barabara katika eneo la Tazara, Jijini Dar es salaam. “Tuko tayari kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza Mpango wake wa Pili wa Taifa wa Maendeleo kwa kuwekeza fedha katika miradi mbalimbali ya maendeleo mliyoipa kipaumbele kuiwezesha nchi kufikia malengo yake ya kuwa nchi ya viwanda ifikapo mwaka 2025” alisisitiza Makamu huyo wa Rais wa JICA.
Ameahidi kuwa Shirika lake pia linaagalia uwezekano wa kuishirikisha sekta binafsi nchini Japan kujenga barabara katika eneo la Gerezani ili kupunguza msongamano mkubwa wa magari hasa yanayotoka Bandari ya Dar es salaam na Katikati ya Jiji la Dar es salaam.
Kwa upande wake Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango, ameeleza kuwa uhusiano kati ya Japan na Tanzania ni wa muda mrefu na kwamba nchi hiyo imekuwa mdau wake mkubwa wa maendeleo.
Amesema katika mazungumzo kati yake na Makamu huyo wa Rais wa JICA, wamekubaliana kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa barabara eneo la Bendera tatu na Gerezani ili kupunguza msongamano wa magari kutoka katikati ya Jiji la Dar es salaam “Mradi Mwingine ni ujenzi wa barabara kutoka eneo la Moroco hadi Mwenge, Jijini Dar es salaam, ambayo Japan waliahidi kuijenga muda mrefu uliopita” Aliongeza Dkt. Mpango
Amesema kuwa wamekubaliana pia kwamba Shirika hilo lisaidie kufungua ukanda wa Kati kwa kujenga barabara ya Kigoma-Nyakanazi na Kigoma-Mto Malagarasi, ambazo hazijapata mfadhili mpaka sasa.
“Halikadhalika nimemwomba atusaidie kuhamasisha sekta binafsi nchini Japan kuja Tanzania kuwekeza katika sekta ya viwanda vya kutengeneza dawa na vifaa tiba ili kuokoa kiasi kikubwa cha fedha ambacho serikali inatumia kuagiza dawa nje ya nchi na pia itakuwa chanzo cha ajira kwa vijana” alisisitiza Dkt. Mpango
Waziri huyo wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, ametaja eneo lingine kuwa ni kuiomba Japan iongeze fursa ya mafunzo kwa vijana wa kitanzania katika nyanja za tiba na ujuzi maalumu ambao haufundishwi hapa nchini.
Amesema kuwa ameiomba pia nchi hiyo ya Japan iendelee kusaidia sekta ya kilimo inayotegemewa na idadi kubwa ya watanzania kwa kusaidia kuongeza uzalishaji na kusindika mazao ya wakulima ili kuyaongezea thamani.
Katika majadiliano hayo, Makamu wa Rais wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan Noriko Suzuki, aliiomba Serikali ya Tanzania itoe msamaha wa kodi kwa miradi miwili mikubwa inayotekelezwa na wakandarasi mbalimbali kupitia shirika hilo ikiwemo ujenzi wa barabara ya Bagamoyo na mradi wa maji mkoani Tabora, maombi ambayo amesema Serikali itayafanyiakazi.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA