Mwenyekiti
wa Chama cha Umma (Chaumma), Hashim Rungwe amesema kinachoonyeshwa na
Rais John Magufuli katika kazi zake ni tabia zake binafsi, badala ya
utendaji.
Rungwe, ambaye aligombea urais mwaka jana na kushika nafasi ya tano
akiwa amepata asilimia 0.32 ya kura, alisema hayo alipofanya mahojiano
na gazeti hili ofisini kwake jijini.
Rungwe alikuwa akizungumzia mwaka mmoja wa Magufuli, akisema
kinachofanywa na Rais pamoja na wateule wake ni kutaka kuonyesha
wanafanya vizuri kuliko watangulizi wao.
“Nasikia kelele na ukosoaji wa kila kilichofanywa kabla ya utawala huu.
Ni hulka ya binadamu kudhani kuwa kila wazo lake ni bora kuliko wengine
na atapenda kulitekeleza, hata ikimaanisha kwenda kinyume na taratibu
zilizopo,” alisema Rungwe.
Pamoja na mtazamo huo, Rungwe alikiri kuwapo kwa maendeleo yaliyotokana
na juhudi binafsi kwa kila mwananchi, huku akikosoa mambo mengi
yanayofanywa na ama Rais mwenyewe au wasaidizi wake.
Alikumbusha kauli aliyoitoa Rais wakati akihutubia mkutano wa hadhara
uliofanyika kisiwani Unguja kushukuru wananchi kwa kumchagua kwenye
Uchaguzi Mkuu uliopita kuhusu kitendo cha katibu mkuu wa CUF, Maalim
Seif Sharif Hamad kukataa kumpa mkono Rais wa Zanzibar, Dk Mohammed
Shein kwenye mazishi ya aliyekua Rais wa Awamu ya Pili wa Zanzibar,
Abood Jumbe.
Siku hiyo, Rais Magufuli alisema: “Mtu mmekutana kwenye msiba, mahali
kwenye majonzi, mnamsindikiza marehemu. Kwa unyenyekevu wako Dk Shein
ukatoa mkono wako kumsalimia mtu fulani. Huyu mtu akakatalia mikono yake
na bado asubuhi yake ukasaini fomu zake za kwenda kutibiwa nje ya nchi.
“Haya ni mapenzi makubwa sana. Amekataa mkono wako. Huyohuyo akiugua
unampeleka hospitali. Akitaka kusafiri nje, unasaini na unampa na fedha
na posho za kwenda nje. Mimi nisingeweza.”
Pia Rungwe alikumbusha pia tukio lililojiri wakati wa uzinduzi wa Daraja
la Nyerere ambako Rais aliwauliza wananchi kama amtumbue au asimtumbue
aliyekuwa mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, marehemu Wilson Kabwe.
“Hizi ni tabia binafsi. Hatuhitaji kuzifahamu. Tunataka uongozi kwa
kutumia sheria tulizonazo. Rais hafahamu tofauti hiyo. Urais ni tofauti
na tabia zake ambazo anaweza akazifanya akiwa na familia yake au watu
wake wa karibu,” alisema wakili huyo wa Mahakama Kuu.
Alisema kauli ya Rais kwamba angekuwa yeye asingesaini kuidhinisha
malipo ya safari ya matibabu ya Maalim Seif baada ya kukataliwa kutoa
mkono wa salamu, haina maana kwa kuwa hasira humpata mtu yeyote na si
vyema kuzionyesha mbele ya watu.
“Rais kuonyesha hasira kiasi hicho si vizuri. Maalim alikuwa kiongozi wa
nchi hii na anayo haki kwa kila analostahili, si mpaka amfurahishe mtu
fulani,” alisema Rungwe na kufafanua kuwa hali hiyo ya kutaka
kufurahisha ndiyo inayosababisha kila mtu ajaribu kumfurahisha Rais hata
kwa kuvunja haki za wengine.
Alisema ipo mifano hai ya viongozi waliokuwa na nia njema ya kuwasaidia
wananchi wao, lakini wakashindwa kufanikisha malengo yao.
“Rais Magufuli anaelekea huko hivyo washauri wake wachukue hatua mapema kabla mambo hayajaharibika,” alisema Rungwe.
Mwenyekiti huyo wa chama ambacho hakijapata uwakilishi bungeni, alisema
hata Rais wa Awamu ya Kwanza, Mwalimu Julius Nyerere alikuwa na nia
njema ya kuijenga Tanzania ya ujamaa na kujitegemea hadi akaasisi Azimio
la Arusha, lakini hakufanikisha ndoto yake.
Alitaja mfano mwingine kuwa ni Zimbabwe ambako uchumi unayumba kutokana
na sera zinazotekelezwa na Rais Robert Mugabe. Alisema alipoikuta nchi
hiyo ni tofauti na alipoifikisha.
“Nilienda Zimbabwe, hali ni tofauti sana. Uchumi umeharibika kutokana na msimamo wa Rais,” alisema.
Miongoni mwa masuala ya kiuchumi yaliyobadilisha uchumi wa taifa hilo,
kwa mujibu wa Rungwe, ni kutaifisha mashamba makubwa ya walowezi na
kuyagawa kwa wakulima wazawa jambo, lililolalamikiwa na wengi.
Kutokana na mifano hiyo, Rungwe alimtaka Rais Magufuli kukumbuka
mahitaji ya wananchi wote badala ya kuelekeza nguvu nyingi kupambana na
kundi dogo la wezi kwenye jamii.
Alisema licha ya uzuri wa kupambana na wizi, rushwa na matumizi mabaya
ya viongozi, wananchi wengi wana njaa ambayo haiwezi kumalizika kama
hakutakuwa na chakula mezani kwao.
“Wezi na wala rushwa wameandikwa hata kwenye vitabu vitakatifu. Lazima
wawepo kwenye jamii yoyote, lakini huwezi kuwatafuta wezi 100 na
kuathiri maisha ya zaidi ya Watanzania milioni 50,” alisema.
“Mishahara haijaongezeka, pensheni hazilipwi kwa wakati lakini wateule
wote wa Rais wanaishi maisha mazuri. Wamebadilika tangu walipoteuliwa.
Wengine walikuwa wanafunzi, lakini sasa wanaongea lugha tofauti.
Wananchi wanahitaji chakula mezani si vita visivyokuwa na mwisho,”
alisema.
Utumbuaji
Kuhusu utumbuaji, Rungwe alisema umekuwa ukifanywa kinyume na taratibu,
jambo alilosema linaongeza chuki miongoni mwa watumishi na Serikali yao.
“Utumbuaji unatengeneza chuki baina ya watumishi wa umma na mwisho wa
siku Rais awe tayari kuwaomba radhi watumishi anaowatumbua,” alisema.
Alielekeza lawama kwa washauri wa Rais kwamba hawatekelezi wajibu wao
kama inavyotakiwa ndiyo maana anaweza kuongea vitu ambavyo haviendani na
hadhi ya ofisi anayoihudumu.
“Rais ni kama baba wa familia. Hawezi kumdhalilisha mbele ya kadamnasi
mwanaye aliyekosea. Wanachofanyiwa watumishi na wafanyabiashara si
sahihi. Ndiyo maana hawajafikishwa mahakamani. Wapo watumishi
wanaoendelea kulipwa mishahara na hawafanyi kazi,” alisema.
Katiba Mpya
Alisema Rais Magufuli hajaonyesha nia ya kukamilisha mchakato wa kuipata
Katiba Mpya ambao ulianza wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne na
ukasitishwa kupisha Uchaguzi Mkuu.
“Rais hatakiwi kusitisha mchakato huo ambao ulianzishwa kwa baraka za
chama chake na Watanzania wote wamekubali fedha zao zitumike kufanikisha
hilo. Katiba na sheria ndizo zilizompa nafasi ya kuongoza nchi na si
kitu kingine,” alisema.
Ila, alikosoa utaratibu uliotumiwa na Bunge Maaalum la Katiba (BMK)
kupitisha Katiba inayopendekezwa kwa kupiga kura, akisema haikuwa
sahihi.
“Tulijaa wanasiasa. Maamuzi yetu yalitokana na itikadi zetu. Katiba si
suala la chama. Marekebisho yafanywe kuanzia pale,” alishauri.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA