KAMANDA wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro, ametaja
mambo matatu ikiwamo siasa kuwa yanakwamisha jitihada zao.
“Kuna tofauti kubwa kati ya siasa na masuala ya ulinzi na usalama, watu
wasichanganye haya,” amesema Kamanda Sirro kwenye mahojiano maalumu juzi
na gaeti hili.
Hata hivyo, alisema Jeshi lake linafanya juhudi kubwa kukabiliana na uhalifu Dar es Salaam.
Kamanda Sirro alisema haipaswi watu kuchanganya siasa na utendaji kazi wa Jeshi hilo.
Sirro alitoa kauli hiyo huku kukiwa na mvutano na mkanganyiko kati ya
Jeshi hilo na baadhi ya vyama vya siasa, kuhusu kuzuiwa na kuruhusiwa
kufanya mikutano ya kisiasa.
Kamanda aliyepokea kijiti kutoka kwa mtangulizi wake, Suleiman Kova
aliyestaafu hivi karibuni, alitaja mambo mengine mawili yanayokwamisha
Polisi kuwa ni uzushi juu ya uporaji unaodaiwa kufanywa na vikundi na
wananchi kushindwa kutoa ushahidi mahakamani dhidi ya wahalifu.
“Wapo wanaohusisha ulinzi na usalama na mambo ya siasa. Yaani utakuwa
ukizungumzia suala la vikundi vya ulinzi shirikishi wao (wananchi)
wanapinga na kudai haiwahusu kwa kuwa ni wanachama wa chama fulani,”
alisema.
“Katika uhalifu hakuna anayeulizwa ‘wewe ni wa chama gani’. Siasa ibaki
siasa na usalama uwe usalama. Ulinzi na usalama ni jambo la kila mtu.
Siasa itumike kulinda na kuleta amani na utulivu na si kuharibu amani na
utulivu,” alisisitiza.
Katika suala hilo hilo la siasa, Kamanda Sirro aliulizwa juu ya tuhuma
zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam, Paul Makonda kudai alipokea rushwa ya Sh milioni 50 kutoka kwa
kikundi cha wafanyabiashara 10 wa shisha, ili waendelee na biashara
hiyo, ambapo alionesha kushangazwa.
Kamanda huyo alisema: “Sina jibu kuhusu shisha. Ila tunaendelea kukamata wafanyabiashara wa shisha.
“Nimezunguka sana hii Dar es Salaam. Nikiwa na nyota moja nilikuwa
Oysterbay, baadaye nikaenda kuwa CID (Ofisa Upelelezi Makosa ya Jinai
Wilaya) Kawe na baadaye Wazo, nimekuwa OCS Kijitonyama mpaka Mkuu wa
Upelelezi Msaidizi wakati wa Gewe (Alfred-Kamanda wa Polisi Dar), kisha
nikaenda Chang’ombe, lakini sikuwahi kusikia shisha,” alisema.
Alisema licha ya kuelezwa kuhusu shisha aliahidi kupambana na wahusika
huku akikiri wazi kuwa hakuwa akijua kilevi hicho na kubainisha kuwa
huenda kimeibuka nchini miaka ya hivi karibuni.
“Hata makamanda wenzangu waliopita sidhani kama walikuwa wanaijua shisha. Inaonekana ipo kwenye hoteli kubwa,” alisema.
Hata hivyo, alisema kwa amri iliyotolewa na Makonda ambaye ni Mwenyekiti
wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na ni bosi wake, lazima
operesheni hiyo ifanyike na wahusika wakamatwe.
“Mfano mpaka sasa tumeshawakamata watu watatu na baadhi ya mitambo yao
na tutaipeleka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kuona madhara yake halafu
baadaye watapelekwa mahakamani,” alisema.
Aliongeza: “Mkuu wa Mkoa amenielekeza na amekuwa ananielekeza kukamata
shisha na makosa mengine kwa kuwa ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi
na Usalama. Ninafanya hivyo kwa moyo mkunjufu.”
Alisema baada ya kuibuka matukio ya makundi ya vijana wadogo, kama Panya
Road, Mbwa Mwitu na Watoto wa Mbwa, wakati mwingine kunaibuka uvumi
mitaani juu ya makundi hayo kuvamia mtaa akisema:
“Wakati mwingine tunafuatilia na kubaini kuwa ni uzushi tu.”
Alitaja kikwazo kingine kuwa ni wananchi kusita kutoa ushahidi
mahakamani, jambo linalosababisha watuhumiwa kuachwa huru na kurejea
tena mitaani.
“Kwenye uhalifu hasa wa makosa ya kubaka, hatupati mafanikio maana
wananchi hawatoi ushahidi na hata wazazi nao wakati mwingine si
wafuatiliaji sana. Unapotoa ushahidi mtu akafungwa miaka 30 mpaka atoke
atakuonea wapi?” Alihoji.
Sirro alisema tangu ateuliwe kushika nafasi hiyo Februari 15,
amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kudhibiti waliokuwa wakitikisa Jiji huku
akitaja mambo saba yaliyosaidia kupunguza uhalifu.
Alisema mafanikio ya Jeshi hilo kwanza yalitokana na nidhamu ya askari
wake, akibainisha kuwa ndicho chanzo cha Polisi kukusanya Sh milioni 95
kutokana na makosa ya barabarani kwa siku.
“Mfano askari wa kikosi cha usalama barabarani waliokwenda kinyume na
maadili tuliwaondoa. Askari wenye tuhuma ambazo hazina ushahidi
tumewahamisha. Pia tuna kamati ya maadili ambayo hufuatilia utendaji wa
kila askari,” alisema.
Alisema mambo mengine ni wananchi kutambua umuhimu wa ulinzi shirikishi,
kukamatwa kwa silaha akitolea mfano silaha 25 zilizokamatwa hivi
karibuni katika tukio la polisi kurushiana risasi na majambazi na
kusababisha kifo cha askari mmoja.
“Majambazi wengi wamekamatwa na wengine kuuawa. Tumeimarisha vikosi
vyetu vya kupambana na ujambazi na wizi wa magari. Hivi sasa ukiiba gari
hufiki mbali utakamatwa tu,” alisema.
Alizungumzia kuibuka kwa matukio ya watoto wadogo kufundishwa mbinu za
uhalifu, Sirro alisema lengo ni wanaowafundisha kuwatumia kujipatia
kipato.
“Wakati mwingine utakuta mzazi ni mhalifu na anamfundisha mtoto mbinu.
Tunapowabaini wazazi tunawachukulia hatua, ila watoto wapo wanaoweza
kupelekwa kwenye mahakama za watoto na vituo vya ushauri nasaha,”
alisema.
Akizungumzia usalama Dar es Salaam, Kamanda Sirro alisema Polisi
imedhibiti kwa kiasi kikubwa uporaji fedha kwa wananchi wanaotoka benki,
uvamizi katika vituo vya Polisi, dawa za kulevya na kudhibiti vikundi
vya uhalifu.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA