Kutokana na taarifa hiyo, Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA)
umebainisha katika ripoti hiyo kuwa baada ya mawasiliano baina ya
wakaguzi na kampuni hizo, ilionekana kodi hizo zina mgogoro na tayari
imeishaifahamisha Mamlaka ya Mapato Tanzania
Dar es Salaam. Ripoti ya ukaguzi wa kampuni za madini nchini ya mwaka
2015 imebainisha kutolipwa kwa kodi za Sh521.6 bilioni kutokana na
kuwapo mazingira ya udanganyifu katika malipo na shughuli za uzalishaji.
Kutokana na taarifa hiyo, Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA)
umebainisha katika ripoti hiyo kuwa baada ya mawasiliano baina ya
wakaguzi na kampuni hizo, ilionekana kodi hizo zina mgogoro na tayari
imeishaifahamisha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard
Kayombo aliliambia gazeti hili jana kuwa hajaiona ripoti hiyo hivyo
asingeweza kuzungumza lolote.
Taarifa hiyo imeonyesha kuwa kampuni za madini zimekuwa zinaingiza
matumizi yasiyostahili katika gharama za uzalishaji wakati wa ukokotoaji
wa kodi. Matokeo yake, Dola za Marekani 46,096,634 zimepotea.
Pia, zimeingiza gharama ambazo hazikutakiwa wakati wa uzalishaji (Dola
95,236,673) na kulikuwa na kodi za mishahara (PAYE) na ujuzi (SDL)
ambazo hazikulipwa wakati wa malipo ya mishahara (Dola 1,278,444) na
kodi zilizotokana na shughuli za kampuni za huduma, malipo ya
menejimenti (Dola 96,687,245). Jumla ya fedha hizo ni Dola za Marekani
239,298,996, sawa wastani wa Sh521.5 bilioni.
Bila kutaja kampuni husika, ripoti hiyo ya TMAA inasema baada ya mvutano
baina ya wakaguzi na wakaguliwa, kodi hizo ndizo zilibaki bila
makubaliano na hivyo kuwasilishwa TRA.
Pia TMAA imebainisha kuwapo kwa Sh10,274,249,769 ambazo pia hazikulipwa
katika mrabaha (Sh7,791,709,388) na ushuru wa huduma Sh2,482,540,381.
Mwaka 2014, shirika la kiuchumi lenye makazi yake Marekani (GFI),
lilitoa ripoti yake likieleza kuwa Tanzania hupoteza zaidi ya Sh3
trilioni kila mwaka kutokana na ukwepaji kodi unaofanywa na kampuni za
uchimbaji.
Makamu wa Rais wa Kampuni ya Acacia, Deo Mwanyika ingawa alisema ripoti
hiyo hajaiona, alipinga matumizi ya maneno ‘udanganyifu’ wa ‘kukwepa
kodi’.
“Nikiipitia ripoti hiyo ndiyo naweza kueleza sisi tunatakiwa kufanya
nini kwa sababu yako mambo mengi, ukokotozi wa gharama za uzalishaji
umekuwa na migogoro na ndiyo maana kuna mahakama za kuomba tafsiri.
Lakini siyo sahihi kuita ukwepaji kodi,” alisema.
Mwanyika alisema kampuni inapofanya ukokotoaji wake wa gharama za
uzalishaji zinaweza kuwa tofauti na tafsiri ya ukokotoaji wa Serikali.
Hata hivyo, alikiri kuwapo uwezekano wa kampuni kukwepa kodi endapo
itakuwa inafanya kazi na kampuni zake yenyewe kupitia ununuzi na mikopo.
“Sisi Acacia hatuna kampuni nyingine wala benki tunayojikopesha mikopo
ila kama kuna kampuni hizo basi ni rahisi kuwapo mazingira hayo,”
alisema.
Kwa mujibu wa tafiti na uchambuzi wa wataalamu mbalimbali wa madini,
kampuni nyingi za madini zimekuwa zikitumia njia ya kupandisha gharama
za uzalishaji na kupunguza bei ya mauzo katika masoko ili kukwepa kodi
kwa njia ya kujirudishia gharama isivyokuwa halali.
Katika mazingira ya ukwepaji kodi, kampuni hizo hutumia kampuni dada ili
kujiuzia mitambo au kujikopesha kwa riba kubwa. Gharama hizo huingizwa
katika ukokotoaji kama garama za uzalishaji.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA