*Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu asafiri kuelekea Mwanza na ndege ya Air Tanzania kama abiria wa kawaida*
==========
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan
amewasili jijini Mwanza na kwa mara ya kwanza umetumia usafiri ya ndege
ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) aina ya bombardier Q400 kutoka
Dar es Salaam hadi Mwanza ambapo ndege hiyo pia ilibeba abiria wa
kawaida katika safari hiyo.
Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na waandishi wa habari
katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es
Salaam kabla ya kusafiri na baada ya kuwasili mkoani Mwanza amewahimiza
wananchi kutumia usafiri wa ndege za ATCL kwa sababu ni wa bei nafuu na
usafiri wake ni wa uhakika.
Amesema kwa kutumia ndege ya ACTL imemsaidia kupunguza gharama kubwa ya
usafiri kwa kutumia ndege za binafsi za kukodi kwa ajili ya safari za
kikazi za ndani ya nchi.
“Ni ndege zetu ni fahari yetu zipo Tanzania ni lazima sisi Watanzania
tuzitumie ipasavyo kusafiria ndio maana na mimi leo nimeamua kutumia
usafiri wa ATCL kwa sababu ni mzuri na wa uhakika”
Makamu wa Rais amesema amefurahi kusafiri kwa mara ya kwanza na ndege
hiyo kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza na amehimiza viongozi na wananchi
kwa ujumla kutumia usafiri wa ndege za ATCL ili kulipa nguvu shirika
hilo katika ufanyaji wake wa kazi kwa viwango bora zaidi.
Mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege mkoani Mwanza, Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amepokelewa
na viongozi mbalimbali wa serikali na wa vyama vya siasa ambao
waliongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella.
Akiwa mkoani Mwanza, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan atafanya ziara
ya kikazi siku NNE mkoani humo katika wilaya za Ukerewe, Ilemela,
Nyamagana, Misungwi, Kwimba na Magu.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA