Mkapa Ampongeza Jk Kwa Ujenzi Wa Chuo Cha Udom.

RAIS mstaafu katika serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, amempongeza Rais wa Awamu iliyopita, Jakaya Kikwete, kwa kuthubutu na kuwezesha ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom). 


Akizungumza katika mahafali ya saba ya chuo hicho, alisema Maono ya chuo hicho yalianza na serikali zote tatu ikiwamo aliyoiongoza lakini hakuweza kuthubutu.

“Nampongeza mzee Kikwete kwa kuweza kuthubutu na kufanikisha ujenzi wake na leo tupo hapa.Mradi wa ujenzi wa chuo hichi, uliafikiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) tangu utawala wa Rais wa Awamu ya Kwanza, Hayati Julius Nyerere, Ali Hassan Mwinyi (awamu ya pili) na kisha mimi lakini wote hatukuweza kuthubutu,”alisema Mkapa.

Kadhalika, Rais Mkapa alishauri Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ikutane na kufanya mazungumzo na Vyuo Vikuu vinavyomilikiwa na Serikali ili kuchambua matatizo yanayotokea mara kwa mara. 


Alisema ni vyema uwepo mkutano wa wenyeviti wa vyuo hivyo ili kufahamu gharama wanzotumia kwa ajili ya uendeshaji wake.

Hata hivyo alibainisha idadi ya wanachuo kila kukicha inaongezeka na nakusababisha vyuo hivyo kushindwa kujiendesha, hivyo jambo bora ni kukutana kwa wenyeviti hao na kujadiliana kuhusu gharama za uendeshaji wake.


 Hata hivyo alisema kutoa amri na maagizo kwa wanachuo kila wakati, si suluhisho la kumaliza migogoro vyuoni, lakini pale wenyeviti wa Vyuo Vikuu vyote wakikutana pamoja na kufahamu gharama zao za uendeshaji, kuna uwezekano wa kutatua kero zote.

Naye makamu Mkuu wa Chuo hicho, Prof, Idris Kikula, alisema wahitimu hao wanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji ajira ambayo kwa sasa imekuwa tishio duniani huku akiwashauri kujiajiri na kuacha kutegemea ajira serikalini kutokana na tatizo hilo kuwa la kidunia.
 Mkuu wa Chuo UDOM ambaye ni Rais Mstaafu Benjamin Mkapa akitunuku Shahada mbalimbali katika mahafali ya saba ya chuo hicho.
 Wahitimu wa Mahafali ya saba ya Chuo cha Udom.
Wahitimu wa Shahada ya Uzamili katika Chuo cha Udom wakiwa katika nyuso za furaha baada ya kuhitimu.

Chapisha Maoni

0 Maoni