Maoni: Rais Magufuli Ameleta Heshima Kazini na Adabu ya Fedha

Hakuna binadamu aliyekamilika, zaidi ya Mwenyezi Mungu pekee. Huku wahenga wanasema kila binadamu na mapungufu yake na upekee wake katika dunia hii, ingali kila mtu ana kitu chake cha tofauti ambacho Mwenyezi Mungu kampa ambacho hakifanani na mtu.


Kwanza nichukue fursa ya kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, kwa jitihada zake zote alizofanya tangu aingie madarakani na anazoendelea kufanya kwaajili ya Watanzania kwa ujumla ikiwa lengo na madhumuni yake ni kukamilisha ahadi zake alizoziahidi pindi anapoingia madarakani.

Rais Magufuli ameifanya nchi ya Tanzania kuwa ni nchi ambayo hata viongozi wengine wa nchi jirani wamekuwa wakimsifia kwa utendaji kazi yake hasa katika kukemea mafisadi makazini, kuheshimu kazi, kufanya ziara zake za hapa na pale lengo ni kutaka kuifikisha nchi ya Tanzania mbali na iwe ni nchi ambayo siku moja kila mtu atamani kuishi.

Katika serikali hii ya awamu ya tano nimejaribu kuangalia kuwa kiongozi huyu ni kiongozi ambaye mara nyingi amekuwa akilia na wanyonge ilhali wapo waliokuwa wakijitokeza katika vituo vya runinga mbalimbali wengine wakiwa na ulemavu wa miguu hawawezi kutembea lakini wanatamani kufanya kazi lakini kiongozi huyo amekuwa akiwasaidia kwa kuwapa bajaji ili waweze kuendesha maisha au kusukuma hili gurudumu la maisha, lengo ni kuibadilisha Tanzania.

Hata hivyo tangu ingie madarakani, amekuwa akiwafukuza kazi viongozi ambao hawajitumi katika kazi zao, huku akipiga vita wale ‘wapiga dili’ wanaotaka kupata fedha huku akitumia msemo wa ‘kutumbua jipu’ ambao kila Mtanzania anautambua kwa sasa.

Rais Magufuli amekuwa akiwapunguza wanaoletea mzaha katika kazi za serikali huku akiwasihi kutochezea jasho la wananchi huku akiwaambia hivi wanatakiwa viongozi hao wajue kuwa wao wameajieiwa na wananchi hivyo kuwataka wasibweteke, wafanye kazi zinazowahusu wananchi kama walivyochaguliwa.

Kwasasa hivi viongozi wa nchi wamekuwa wakiiheshimu kazi kutokana na rais Magufuli kuingia ofisi mbalimbali za serikali kwa kushtukiza na muda mwingine hukutana na madudu yanayofanywa na watumishi wa umma ambapo yeye hupinga utendaji kazi huo.

Ziara zake tunaona zimeweza kuzaa matunda katika ofisi mbalimbali ikiwa ni pamoja na bandari ya Dar es Salaam alipofika alikuta kuna upungufu wa mashine hivyo kutaka mashine zingine kuongezwa ili kazi zao waZIfanye kwa weledi na kujua mizigo inayoingia na kutoka katika bandari hiyo.

Pia alipo ingia katika ofisi za gazeti la Uhuru ambapo alipofika pale alikuta wafanyakazi hawalipwi mishahara lakini kazi zikiendelea kutendeka. Pia alifanya ziara ya kushtukiza wakati akimsindikiza uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Nyerere wakati akimsindikiza Rais wa Congo, Joseph Kabila na kufanya mahojiano na baadhi ya wafanyakazi wa eneo lile yaliyomfanya agundue madudu yaliyokuwa yakifanywa na baadhi ya wafanyakazi.

Kwa upande mwingine Rais Magufuli amepigana na kupambana na rushwa si kwamba marais wengine hawakupambana na rushwa, bali yeye kwa kiasi kikubwa amejitahidi na tunaamini ataendelea kupambana na janga hili. Ndio maana hivi karibuni wakati wa mkutano wake na wahariri na waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali vya habari katika nukuu zake nilinukuu akisema ‘RUSHWA NI KANSA YA MAENDELEO YA NCHI‘ huku akisema tuipinge na kuikataa.

Hivi karibuni Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi alisema kila mtu kwa nafasi yake ameipinga rushwa lakini Rais Magufuli ameleta Tsunami katika rushwa na kusema kuwa kwa mwaka mmoja wa rais huyo amewazidi wao kipindi cha nyuma.

Walio chini yake wanajitahidi kwa nafasi zao kufanya ziara zao pia za hapa na pale kwa kufuata kauli mbiu ya uongozi huu ya ‘Hapa Kazi Tu. Hata maneno matakatifu husema asiyefanya kazi na asile kwa hiyo ni vyema kila mtu akapambana kwa nafasi yake kuepuka kuwapa watu lawama.

Kutokana na uongozi wake unaipiga vita rushwam ufisadi na matumizi mabaya ya fedha za serikali, wananchi hususan wafanyakazi wanaiheshimu zaidi fedha wanayoipata kwa jasho kuliko ilivyokuwa awali ambapo fedha za dili ziliwafanya baadhi ya watu waishi kama miungu watu.

Chapisha Maoni

0 Maoni