Katika watu wanaoweza kuelezea kwa mfano halisi kuwa Mungu yupo, ni Christian Longomba ambaye kupona kutoka kwenye upasuaji uliohusisha kupasuliwa nusu ya fuvu lake (kama mtu unavyoweza kupasua boga kutoa mbege za ndani), ni kitu ambacho hadi sasa haelewi iliwezekana vipi.
Muimbaji huyo aligundulika kuwa na uvimbe mkubwa kichwani ambao kama usingetolewa ungeweza kuyakatisha maisha yake tena kwa maumivu makali au kumpa upofu.
Kwenye mahojiano na Mzazi Willy M Tuva jijini Los Angeles wanakoishi kwa sasa, mdogo wake, Lovy Longomba amesema hilo lilikuwa jaribu kubwa katika maisha yao na lilifanya kusimama kwa mipango yote waliyokuwa nayo. Anasema ili kufanyika kwa upasuaji huo, iliwalazimu kusaini makaratasi mengi kuridhia matokeo yote ambayo yangejitokeza baada yake.
Upasuaji huo ulidumu kwa saa 14. Hata hivyo Lovy anasema ilikuwa na kama bahati tu kwasababu kutokana na umri wake aliweza kupona haraka. Chris anasema asilimia 90 ya uvimbe ilitolewa kwa upasuaji na zingine 10 kutolewa na mionzi na hivyo kumfanya apoteze sehemu ya nywele zake za mbele. “Kabla ya kufanyika upasuaji niliambiwa nusu ya mwili wangu unaweza kupooza au utapoteza kumbukumbu zako. Itabidi ufundishwe tena jina lako, jinsi ya kutembea, jinsi ya kula, jinsi ya kutumia bafu kama mtoto tena,” alisema Chris. “Sasa hivi niko fit, kila kitu kiko sawa,” ameongeza.
Hata hivyo Lovy amesema katika wiki ya kwanza, Christian hakuweza kukumbuka mambo mengi japo kitu pekee alichokumbuka ni muziki na kwamba ndio uliomsaidia kurejesha kumbukumbu zaidi.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA