VMM/U.80/8/Vol.I/524/08/2016
Kamati ya Utekelezaji ya Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa CCM Taifa
imekutana Jumatano tarehe 23/11/2016 chini ya Mwenyekiti wake Mhe.
Sadifa Juma Khamis (MCC) (MB) katika ukumbi wa mikutano Makao Makuu ya
UVCCM Dar es Salaam.
Katika kikao hicho cha kawaida pamoja na mambo mengine kimepokea na
kujadili agenda kutoka idara nne za UVCCM Taifa hatimae kufanya maamuzi.
Kamati ya Utekelezaji imeridhishwa na juhudi na mikakati inayoendelea
kuelekea Jumuiya kujitegemea kiuchumi 100% ili kuweza kujiendesha kwa
ufanisi na mafanikio ambapo imeridhia uondoshwaji wa wafanyabiashara
wote waliopo eneo la UVCCM Kinondoni Mwinjuma ili kupisha uvunjaji na
hatimaye kuanza kwa ujenzi wa vitega Uchumi vikubwa katika eneo hilo
ambapo wafanyabiashara waliopo watapewa hati ya siku tisini (90) ili
wawe wameondoka katika eneo hilo. Uwekezaji mpya katika eneo hilo
takriban kwa asilimia 90% utagharimiwa na UVCCM yenyewe.
Kufuatia tathmini iliyofanywa na UVCCM Taifa nchi nzima kwa kutathmini
miradi yake kuanzia ngazi ya Shida hadi Taifa, kamati ya utekeleza
imeamua na kuelekeza kuimarishwa mfumo wa ukusanyaji mapato wa jumuiya
na kusimamia matumizi yake sambamba na kupitia upya mikataba yote ya
uwekezaji kuanzia ngazi ya shina hadi Taifa ili kuepeka mikataba isiyo
na tija kwa taasisi
Kamati ya utekelezaji imejipanga kuongeza uwezo wa taaluma kwa watendaji
wake wote kwa kuwapatia mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu ili
kuwajenga zaidi kitaaluma ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya siasa na
kiuchumi.
Kamati ya Utekelezaji imeziagiza Wilaya na Mikoa kutambua kuwa mali na
Rasilimali za Jumuiya si milki ya mtu au Kiongozi, kila aina ya mali au
kitega Uchumi cha Jumuiya, kinahitaji kulindwa, kutunzwa na kuhifadhiwa
na wanajumuiya wote hivyo imewakumbusha kuanzia sasa ni lazima
kutekeleza Azimio la ?Siasa na Uchumi? kwa vitendo kwa kuzingatia Uchumi
ni Uhai na kipaumbele cha Taasisi yoyote kuweza kujitegemea,
kujiimarisha na hatimae kujiendesha.
Vile vile Kamati ya Utekelezaji imeziagiza ngazi zote zilizopo kwa
mujibu wa Kanuni ya Umoja wa Vijana wa CCM kuhakikisha zinajitathimini
na kuendeleza miradi iliyopo pia kufikiria uibuaji wa miradi mipya
ambapo sifa moja ya mafanikio kwa walengwa ni kuanza kujitathimini jinsi
walivyojipanga katika kufanikisha Uchumi wao na kuepuka kuwa tegemezi
na omba omba.
Kamati ya Utekelezaji imepokea maandalizi ya awali ya Uchaguzi wa Umoja
wa Vijana wa CCM 2017 Ngazi ya Shina, Tawi, Jimbo, Wilaya, Mkoa na Taifa
ambapo Kazi ya kuchapisha kwa wingi na kusambaza kanuni ya UVCCM,
Kanuni ya Maadili ya UVCCM, Kanuni ya Uchaguzi ya UVCCM pamoja na
kuandaa miongozo ya Uchaguzi inaendelea vizuri hivyo imewataka vijana
kuzisoma na kuzielewa vyema kanuni.
Kamati ya Utekelezaji imeridhishwa na maandalizi hayo ya awali na
imeendelea kuwahamasisha Vijana wenye sifa, uzalendo, ukereketwa na
nidhamu ya Chama kujitokeza kwa wingi kuomba kugombea Nafasi za mbali
mbali za Uongozi katika Chama na Jumuiya zake katika Uchaguzi wa 2017.
Kamati ya Utekelezaji imeendelea kuwakumbusha Vijana wote walioonyesha
azma ya kuomba nafasi mbali mbali ndani ya Jumuiya, kuwa kutaka Uongozi
si jambo baya ila ukiukwaji wa Kanuni na taratibu zake ni tatizo hivyo
harakati za kuchafuana, kutengeneza makundi au tishio la kuivuruga
Jumuiya kwa kisingizio cha uchaguzi mwaka 2017 vitendo hivyo
havitafumbiwa macho kwa vile vinaipunguzia kasi ya Utendaji na
utekelezaji wa majukumu taasisi na ifahamike kuwa UVCCM ina Kanuni zake,
Miongozo, taratibu na Maadili hivyo muda huu ni vyema kila mmoja
akaendelea na majukumu yake ya msingi kwa vile kila jambo lina wakati
wake.
Kamati ya utekeleza imeridhishwa na kasi ya ulipaji madeni mbali mbali
ya wastaafu na kulipia mifuko ya Hifadhi ya Jamii ambapo jumla ya T.Shs
205, 456, 754/= zimetumika na wakati huo imeidhinisha matumizi ya T. Sh
209, 918, 250/= na kuelekeza fedha hizo zitumike kulipia mafao ya
watumishi wanaostafu. Hivyo malipo hayo yafanyike haraka iwezekanvyo kwa
wastaafu 35 ambao wamefikia muda wa kustaafu ndani ya UVCCM, aidha
kamati ya utekelezaji imewashukuru na kuwapongeza watumishi hao kwa
mchango mkubwa waliotoa wakati wakiitumikia jumuiya kwa kipindi chote
katika utekelezaji wa majukumu yao ndani ya jumuiya na Chama kwa ujumla.
Kamati ya utekelezaji imepokea taarifa ya uhaba wa madawati katika Mikoa
ya Mara, Simiyu, Rukwa, Kigoma, Geita, Dodoma na Mwanza na imewagiza
makatibu wake wa Mikoa na Wilaya katika mikoa hiyo, kuhakikisha
inasimamia kila kata kutengeneza madawati mawili (2) na kuyakabidhi
wilayani ikiwa ni jitihada za kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali
ya Rais Mhe Dk John Pombe Magufuli za kuimarisha na kuandaa mazingira
bora ya utoaji elimu nchini, hivyo kwa mjumuiko wa kata zilizoko katika
wilaya husika UVCCM itakuwa imekusanya madawati 2136.
Kamati ya utekelezaji imepokea taarifa ya zoezi la uchangiaji wa damu
katika mikoa ya Dodoma , Tabora, Kagera, Katavi, Mwanza na Arusha
iliyofanyika katika wiki ya vijana lengo likiwa kuchangia damu na kuokoa
maisha ya watanzania hasa kina mama na watoto ambapo jumla ya unit
1215.5 zilikusanywa katika zoezi hilo lililozinduliwa na Kaimu Katibu
Mkuu Shaka Hamdu Shaka mkoani Kagera.
Kamati ya utekelezaji ya utekelezaji imepongeza mikoa na wilaya zote
zilizofanikisha zoezi hili na kuitaka mikoa mingine kuendelea na zoezi
hilo kwa vile jukumu hilo ni endelevu kwa kuzingatia UVCCM ni jeshi la
Chama hivyo kazi moja kubwa ni kulinda watu wake hususan katika suala la
afya ya binadamu .
Kamati ya Utekelezaji imetoa baraka zote na kuunga mkono juhudi,
dhamira, malengo na shabaha ya Serikali katika kukomesha zama za
ukwapuzi na Matumizi ya jasho la wengine kwa faida ya wachache.
Kamati ya Utekelezaji imeishauri Serikali kuendelea kufanya kila
linalohitajika kuhakikisha Uchumi wa nchi yetu unajengeka na kuimarika
vizuri zaidi ili kuendeleza mapambano dhidi ya adui ujinga, maradhi na
umaskini.
Mwisho Kamati ya Utekelezaji imempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutekeleza ilani ya uchaguzi wa
CCM ya mwaka 2015/ 2020 na mafaniko makubwa huku akionyesha ushujaa wa
hali ya juu katika kuwapigania na kuwatetea wananchi wanyonge.
*Chief Silvester Yaredi*
*Kny: KATIBU MKUU UVCCM TAIFA*
*24 November 2016*
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA