Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amevunja ukimya kuhusu mgogoro wa uhalali wa Uenyekiti wa Profesa Ibrahim Lipumba anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa unaoendelea ndani ya Chama Cha Wananchi (CUF) ambao umekuwa ukihusishwa naye tangu awali.
Lowassa ambaye alitajwa na Profesa Lipumba kuwa chanzo cha yeye kujiuzulu kabla ya kurejea tena miezi 9 baadae kutengua uamuzi wake, amesema kuwa shida za chama hicho ni shida za vyama vyote vinavyounda Ukawa.
Mwanasiasa huyo mkongwe na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, ametumia ukurasa wake wa Facebook kueleza jinsi ambavyo Ukawa inalibeba tatizo la mgogoro wa CUF.
“CUF ni wenzetu katika Ukawa. Shida zao ni shida zetu, vita vyao ni vita vyetu, kushindwa kwao ni kushindwa kwetu, ushindi wao ni ushindi wetu,” aliandika Lowassa.
Kauli hiyo ya Lowassa imekuja miezi michache baada viongozi wa Ukawa kueleza msimamo wao kuwa hawamtambui Profesa Ibrahim Lipumba kama Mwenyekiti wa CUF na kwamba wataendelea kushirikiana na Katibu Mkuu wa Chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad.
Naye Profesa Lipumba amekuwa akieleza kuwa hayuko tayari kuona Chadema au Lowassa wanakinunua chama hicho.
Hivi karibuni, Ukawa wameweka msimamo wao kuwa watawasimamisha wagombea wa pamoja katika uchaguzi mdogo utakaofanyika mwakani.
Hata hivyo, kumekuwa na changamoto baada ya pande mbili zinazovutana ndani ya CUF kila mmoja kutangaza kuwasimamisha wagombea wake huku Tume ya Taifa ya Uchaguzi ikiweka msimamo kuwa ili iwatambue wagombea wa chama hicho ni lazima fomu zao zisainiwe na pande mbili zinazovutana.
Miezi michache kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, Profesa Lipumba alionekana akimtambulisha Lowassa mbele ya waandishi wabari na kujibu maswali mengi yaliyoelekezwa kwake lakini siku chache baadae alitangaza kujiuzulu akida moyo wake unamsuta hawezi kumuunga mkono mwanasiasa huyo.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA