Serikali ya Jamhuri ya Korea imetoa msaada wa Dola za Marekani elf 50,000 takribani milioni 108 kwa fedha za Tanzania kwa ajili ya waathirika wa tetemeko la ardhi lilitokea mkoani Kagera mwezi Septemba 2016.
Msaada huo ulikabidhiwa leo jijini Dar es Salaam na Balozi wa Korea nchini Tanzania, Mhe. Song Geum Young na kupokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga (Mb) kwa niaba ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa (Mb).
Baada ya kupokea msaada huo, Dkt. Mahiga aliishukuru Serikali ya Korea na kuahidi kuwa msaada huo ataukabidhi kwa Mhe. Waziri Mkuu ili uweze kutumika kama ulivyokusudiwa.
Mhe. Mahiga alisema kuwa Korea imekuwa mbia mkubwa wa Tanzania tokea nchi hiyo ilipoanzisha mahusiano ya kidiplomasia na Tanznaia miaka 25 iliyopita. Alieleza kuwa katika kipindi hicho Tanzania imekuwa ikipokea misaada mbalimbali ya kiuchumi, kijamii na ya kibinadamu ukiwemo huu wa leo ulioelekezwa kwa waathirika wa tetemeko la ardhi la mkoani Kagera.
Mhe. Waziri alitaja misaada ambayo Korea imeipatia Tanzania ni pamoja na ujenzi wa daraja la Malagarasi mkoani Kigoma, ujenzi wa hospitali ya kisasa ya Mloganzila na ujenzi wa hospitali ya uchunguzi wa afya ya Mama iliyopo Chanika. Aidha, Korea hivi karibuni itaanza ujenzi wa daraja la Selander ambalo linatarajiwa kuanzia ufukwe wa Coco, Oysterbay hadi maeneo ya hospitali ya Aga Khan, Upanga jijini Dar es Salaam.
Waziri Mahiga alibainisha pia kuwa Jamhuri ya Korea itatoa msaada mkubwa zaidi wa maendeleo kwa Tanzania kuliko nchi yeyote ya Afrika. Taarifa hiyo ilitolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea, Mhe. Yun Byung-se alipofanya naye mazungumzo kando ya Mkutano wa nchi za Afrika na Korea uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia tarehe 06 na 07 Desemba 2016.
Kwa upande wake, Balozi wa Korea nchini aliahidi kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania hususan kutoa atia misaada ya maendeleo ili iweze kutimiza azima ya Serikali ya awamu ya tano ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 27 Desemba 2016.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA