Mke wa Yeriko Nyerere, (kada wa Chadema) Neema Alex amesema mumewe ameshindwa kufikishwa mahakamani jana kutokana na kutokamilika kwa baadhi ya mambo.
Hata hivyo, Neema hakuwa tayari kutaja kilichokwamisha Yeriko kufikishwa mahakamani na kusema kila kitu kiliandaliwa na nyaraka zote zilikuwa tayari kwa ajili ya Yeriko kufikishwa mahakamani.
“Wakati tukimsubiri atoke na kuelekea mahamakani ghafla simu ikapigwa na mmoja wa wakubwa wa polisi akitoa amri ya kwamba asipelekwe mahakamani hadi atakapopiga simu tena.
“Nahisi bado hawajaridhika na maelezo aliyoyatoa mume wangu (Yeriko) ingawa sina uhakika,” alisema Neema wakati akizungumza kwa simu na gazeti hili jana.
Yeriko alikamatwa saa tisa alfajiri juzi akiwa nyumbani kwake Mbutu, Kigamboni na watu wanaodaiwa kuwa maofisa usalama wa mitandao kisha kumpeleka katika Kituo Kikuu cha Polisi cha Kanda Maalumu.
Katika tukio hilo, maofisa hao waliambatana na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mbaragande, Jamal Hassan anakoishi Yeriko. Neema alisema kuwa jana wakiwa na baadhi ya viongozi wa Chadema walikwenda Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa ajili ya kumsubiri mumewe ambaye hakupelekwa kama walivyotarajia.
Hata hivyo, Neema alisema alifanikiwa kuonana na kuzungumza na Yeriko ambaye alisema yupo katika hali nzuri na hana wasiwasi wala tatizo lolote.
Wakili wa Yeriko, Peter Kibatala alisema hadi jana mchana hakupata taarifa zozote kutoka polisi kwa kuwa alikuwa na majukumu ya kushughulikia kesi nyingine.
“Sijui chochote kwa sasa? Kwa sababu asubuhi niliamkia mahakamani kwa ajili ya kesi ya Lissu (Tundu-Mwanasheria wa Chadema),” alisema Kibatala.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Mbaragande, Hassan alilieleza juzi kuwa maofisa hao walimwambia wanamkamata Yeriko kwa sababu ya makosa ya mtandao.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA