Profesa Ibrahim Lipumba Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF)
aliyefutwa uanachama na Baraza Kuu la Uongozi Taifa la Chama hicho,
amesema usaliti uliofanywa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) kwa aliyekuwa Katibu Mkuu wake Dkt. Wilbroad Slaa na kukiuka
makubaliano ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) katika kipindi cha
kampenzi za uchaguzi mkuu wa 2015 utakigharimu chama hicho.
Lipumba ameyasema hayo Novemba 26, 2016 katika mkutano wake na baadhi ya
viongozi wa kata za Jimbo la Temeke kwenye Ukumbi wa Sunrise ulioko
Tandika jijini Dar es Salaam.
“Usaliti wa Chadema kwa Dkt. Slaa utaendelea kuigharimu na ndio maana
hawataki nirudi katika wadhifa wangu na nikirudi watakwisha,” amesema.
Amedai kuwa, usaliti wa Chadema umesababisha upinzani kupokonywa ajenda
yake ya ufisadi na kuruhusu Rais John Magufuli kuitumia ajenda hiyo
kumaliza nguvu ya upinzani.
“Rais Magufuli ametunyang’anya ajenda ya kusimamia ufisadi, leo hii
Chadema hawana ajenda ya kupinga ufisadi kwa sababu ya kumuasi Slaa,” amesema.
Kuhusu Ukawa Lipumba amedai kuwa, baadhi ya viongozi wa Chadema
wanautumia umoja huo kuiua CUF Bara huku akituhumu baadhi ya viongozi wa
CUF kuwa wananjama za kukiuza chama hicho.
Aidha, amesema alifikia hatua ya kujizulu mwezi Agosti mwaka jana
uenyekiti wa CUF kwa madai ya kutokubaliana na hali ya kuwa mpiga debe
wa Edward Lowassa aliyekuwa mgombea wa kiti cha urais kwa tiketi ya
Chadema na mwamvuli wa Ukawa.
“Nilikataa kuwa mpigadebe wa Lowassa, niligombea urais mara nne leo
hii nisimame kumpigia debe Lowassa? Ambaye kwenye orodha ya majina ya
mafisadi jina lake lilikuwa namba nmoja. Nisingeweza fanya hivyo nikaona
bora kujiudhuru,” amesema.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA