Dar es Salaam. Siku tatu baada ya kudaiwa kumfanyia fujo jirani yake,
Mchungaji wa Kanisa la Maombezi (GRC), Anthony Lusekelo maarufu Mzee wa
Upako, amejibu tuhuma hizo akisema anaishi kana kwamba hana jirani.
“...Tunaishi kama majambazi tu, hujui jirani yako ni nani,” amesema.
Lusekelo amesema Yesu ambaye ni mwana wa Mungu alikubali kudhalilishwa
na baadaye kufa bila hatia hivyo na yeye alikubali kula kiapo katika
nafasi ya utumishi wake. Amesema magazeti hayawezi kumshusha kwa kuwa
hayakumpaisha ila Mungu pekee.
Katika mahubiri yake yaliyohudhuriwa na waumini wengi kama ilivyo kwa
Jumapili nyingine za karibuni kanisani kwake, Ubungo Kibangu, mchungaji
huyo aliingia kwa mapokezi ya wimbo wa kuabudu uitwao ‘Angalia Bwana’
kabla ya waumini kuanza kumtunza kwa sadaka kama ilivyo kawaida ya ibada
zake.
Alhamisi iliyopita, mitandao ya kijamii ilikuwa na picha zinazomuonyesha
Mzee wa Upako akirushiana maneno makali na jirani yake lakini mchungaji
huyo hakupatikana kuzungumzia tukio hilo ambalo lilisambaa baada ya
mwandishi wa habari, Happiness Katabazi aliyeshuhudia mzozo huo,
kuandika kwa kirefu kisa hicho na kusambaza kwenye mitandao ya kijamii.
Picha ya video iliyosambaa mitandaoni ilimuonyesha mtu anayedaiwa kuwa
ni mchungaji Lusekelo akijibizana na sauti ya mwanamke, ambaye
haonekani, huku gari la rangi nyeusi aina ya Toyota Landcruiser likiwa
limeegeshwa katikati ya barabara ya mtaani na kuzuia mengine kupita.
“Kwanza waliandika habari kwamba waumini hawatakuja kanisani badala yake
wamejitokeza bila kukatishwa tamaa. Wakati mnajitokeza hapa mbele
(kutoa sadaka), alipita mama mmoja amebeba mtoto, nilimwombea mwaka jana
hapa kwamba atapata mtoto na leo amepata mtoto, sasa mbona magazeti
yasiandike habari hizo?”
“Kwanini wasiandike hayo mazuri ‘front page’ (ukurasa wa mbele)?, halafu mnaandika Mzee wa Upako matatani, matatani babu yako.”
“Najua na leo mmekuja mpo humu mnasubiri niseme, nasubiri mmalize kwanza
nyinyi halafu na mimi ndiyo nitasema, baada ya mwezi mmoja najua
mtakuwa mmemaliza", amesema.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA