RC Sadick amnyang'anya shamba mwekezaji



MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro, Said Meck Sadiki, ametoa siku 27 kwa mwekezaji wa Shamba la Kindi Kale, Theo Trading kulirejesha kwa hiyari kwa Chama cha Ushirika cha Mazao (AMCOS), kutokana na kushindwa kuliendeleza kama mkataba unavyoeleza.

Sadiki ametoa agizo alipotembelea mashamba makubwa ya wawekezaji.

Ametoa agizo baada ya kupokea taarifa ya Mwenyekiti wa AMCOS, Peter Swai alipotembelea shamba hilo lililopo Kata ya Kindi wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro.

Amesema hadi kufikia Januari 16 mwaka 2017, mwekezaji huyo awe amerejesha kwa hiyari yake shamba hilo kwa Chama cha Ushirika na Mazao, na endapo atashindwa kutekeleza agizo hilo ndani ya muda aliopewa, atafikishwa mahakamani au kumuomba Rais John Magufuli afute umiliki wa shamba hilo.

Sadiki amesema kilichopo kwenye shamba hilo si uwekezaji bali ni uhuni unaofanywa wa kuhodhi ardhi ya wananchi masikini, bila ya kuwepo uzalishaji wowote wa zao la kahawa, kama masharti ya mkataba yanavyoelekeza.

Amesema kwa sasa hakuna haja ya majadiliano kwa kuwa alichofanya mwekezaji huyo ni kuonesha dharau kwa kukiuka mkataba, hivyo anapaswa kuachia shamba hilo mara moja kabla serikali haijamchukulia hatua za kisheria.

Sadiki pia ameiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Kilimanjaro, kufanya ukaguzi kuona kama mwekezaji huyo alikuwa akilipa kodi ya serikali.

Awali akisoma taarifa ya Maendeleo ya Shamba la Kindi Kale, Swai alisema shamba hilo lenye ukubwa wa ekari 211 limepoteza hadhi kutokana na uharibifu mkubwa wa mazingira, uliofanywa na mwekezaji huyo kwa kukata miti na kupasua mbao na kuni.

Swai ametaja vipengele vingine vya mkataba alivyovunja mwekezaji huyo ni pamoja na kuwakodisha wanachama na wananchi kulima mahindi na maharage, kuruhusu watu kulima kwenye vyanzo vya maji, kutolipa kodi ya serikali, pamoja na kutoisaidia jamii inayomzunguka.

Amesema, mwekezaji huyo ameshindwa kulipa kodi ya pango kwa wakati, ambapo kwa mwaka 2016 anadaiwa zaidi ya Sh milioni 18.4, pia ameshindwa kuonesha ushirikiano kati yake na Bodi ya AMCOS, hata pale anapoandikiwa barua amekuwa hajibu wala hafiki kwenye vikao.

"Tumekwishachukua hatua mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kumwita katika vikao lakini hafiki, pia tumemwandikia notisi mara mbili lakini hakujibu hata moja, naomba serikali iingilie na kumtoa," amesema Swai.

Meneja wa Theo Trading katika shamba la Kindi Kale, Michael Mushi, alisema mwekezaji wa shamba hilo ambaye ni bosi wake amekuwa akiishi Dar es Salaam, ambapo amekuwa akimfikishia barua zinazotoka AMCOS lakini amekuwa hatoi majibu wala kuhudhuria vikao vya bodi hiyo anapohitajika.

Chapisha Maoni

0 Maoni