Dawa za kisukari zaadimika mahospitali, serikali yakiri upungufu huo

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema kuna tatizo la upatikanaji wa dawa kwa wagonjwa wenye kisukari hivi sasa linaloikabili nchi na juhudi zinafanyika kulitatua.


Waziri ametoa kauli hiyo baada ya kupata malalamiko kutoka kwa wananchi wa kata ya Mkula wilaya ya Busega mkoani Simiyu wakati wa mkutano wa hadhara, ambapo walisema huteseka kukosa dawa kwa watu wenye kisukari.

"Naomba nikiri kweli hivi sasa kuna tatizo la upatikanaji wa dawa kwa wagonjwa wenye matatizo ya sukari nchini, lakini mikakati mbalimbali tumeweka kwa ajili ya kuweza kupambana nalo," amesema.

Amesema, wizara imepitisha mkakati wa kupambana na magonjwa yasiyoambukizwa, kikiwemo kisukari, ambapo huduma za kisukari zitaanza kupatikana kuanzia ngazi za vituo vya afya kuliko hivi sasa huduma hizo wanazipata kwenye hospitali kubwa kama Bugando.

Waziri huyo alieleza kuwa kupitia mkakati huo, dawa pamoja na huduma nyingine kwa magonjwa hayo kikiwemo kisukari, zitaanza kupatika katika ngazi hiyo lengo likiwa kuanza kupamba na magonjwa hayo ngazi ya chini.

Hata hivyo, aliwataka watanzania kutambua kuwa kinga ni bora kuliko tiba, kwa kufanya mazoezi mara kwa mara, kutokula vyakula kwa mazoea, ikiwa ni pamoja na kutokunywa pombe kupita kiasi.

Chapisha Maoni

0 Maoni