Juma Kaseja afunguka mengi kuhusu Simba na Kurudi Yanga

Kipa mkongwe, Juma Kaseja. 

KUNA dhana ipo akilini mwa wapenda soka wengi kuwa umri wa kipa unavyozidi kuwa mkubwa ndivyo kiwango kinazidi kuwa bora.


Mifano ipo mingi ndani na nje ya Tanzania, kwa hapa nchini mfano wa karibu ni kwa mkongwe, Juma Kaseja ambaye amedumu kwenye soka la Bongo kwa zaidi ya miaka 15.

Kaseja amefanikiwa kukaa juu kwa muda mrefu huku silaha yake kubwa ikiwa ni katika upanguaji wa mikwaju ya penalti.

Kipa huyo ambaye alikuwemo kwenye kikosi cha mwisho cha Simba kilichotwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2011/12, kwa sasa anakipiga ndani ya kikosi cha Kagera Sugar chini ya Kocha Mecky Maxime.

Bado inaaminika kwamba yupo kwenye kiwango cha juu, kipa huyo ambaye ni baba wa watoto wawili kwa mkewe, Nasra Nassor, amezungumza na Championi Ijumaa, hivi ndivyo alivyofunguka:

“Kwanza nashukuru kumaliza msimu wa ligi salama huku tukiiwezesha timu yetu kufikia mafanikio haya ambayo tunayo kwa sasa ya kumaliza nafasi tatu tena tukiwa ndiyo timu pekee kutoka nje ya Dar kuwa ndani ya nne bora.

Maisha ya Kagera Sugar kwako yakoje?

“Nisiwe muongo, kwa muda ambao nimedumu hapa naomba niseme ni mahali pazuri kwa mchezaji ambaye anataka mafanikio maana ni sehemu isiyo na majungu bali ubora wa kazi yako ndiyo unakupa nafasi ya kucheza na utaona kukunjua roho ya kila mchezaji ndiyo kumetufanya tufikie mahali hapa.

Unamaliza mkataba, nini kinafuata?

“Ni kweli mkataba wangu na Kagera unaisha, lakini wao nawapa nafasi ya kwanza kwa sababu wamenirudisha katika sehemu ambayo wengi waliona siwezi kuifikia.

“Unajua pia Kagera wana utamaduni wao, ukiangalia wachezaji wote tuna mikataba ya muda mfupi yaani mwaka mmoja au miwili ambapo inakupa nafasi ya wewe kama unamaliza basi unaangalia maisha yako mengine.

Kwa hiyo unataka kusema utaondoka?

“Inaweza kuwa hivyo kwa sababu niko huru kuamua juu ya hatma ya maisha yangu lakini kipaumbele cha kwanza ni juu ya timu yangu ya sasa kisha wengine ambao wanataka kunisajili basi waje tujadiliane namna ya kuzitumikia timu zao.

Vipi mipango ya kurejea Simba au Yanga?

“Hakuna kinachoshindikana kujiunga na timu hizo kwa sababu uwezo wangu unajidhihirisha wazi na naweza kucheza lakini nikwambie haiwezi kuwa rahisi kurejea kwao kwa sababu nilipoondoka sikuondoka vizuri na hilo kila mtu analijua sasa wanapotaka kunirejesha basi wasidhani nitakubali kirahisi.

“Lakini pia wakumbuke soka ndiyo maisha yangu, nina familia ambayo inataka mahitaji pamoja na wengine ambao wapo nyumbani Kigoma, wote hao wananufaika kutokana na kazi hii ya soka, hivyo siwezi kukataa kujiunga na timu yoyote ambayo itanipa kile ninachokitaka.

Wamekufuata kuzungumza na wewe?

“Hapana bado hakuna aliyeongea na mimi, nadhani kwa sababu ndiyo kwanza tumemaliza msimu hivyo wanajipanga lakini hata mimi najipanga kufanya mambo yangu.

Nini siri ya kiwango chako?

“Ni mazoezi tu na kutokuwa na mambo mengi nje ya uwanja, unajua wengi wanashindwa kutamba muda mrefu kwa sababu wana vitu vingi ambavyo wanavifanya nje ya uwanja tofauti na mimi Juma ambaye nikimaliza mambo ya soka narejea nyumbani.

“Pia mazoezi kwa wingi na kujitunza mwili hapa wengi wanafeli kwa kushindwa kuitunza miili yao unakuta mchezaji anachanganya mambo mengi kwa wakati mmoja, hivyo ni lazima ufeli na kiwango kishuke.

Baadhi ya mashabiki wanakuona mzee, hilo unalionaje?

“Kwanza nasema kama ningeukubali huo msemo na kuuchukulia ukweli basi hivi sasa Kaseja angekuwa ameshaachana na mpira na anafanya mambo mengine lakini niliukataa na kujiona bado nina nguvu kubwa ya kucheza soka.

“Mashabiki wengi wanawazeesha wachezaji wengi eti kisa mtu kacheza kwa muda mrefu bila ya kuangalia aina ya uwezo wake hasa jambo hilo linatokea ndani ya Simba na Yanga, zenyewe hizo unakuta mtu hata hakujui lakini anasema wewe ni mzee na ukikubali hiyo ndiyo unajimaliza na kustaafu wakati unautamani mpira.

Nini kilichokuondoa Mbeya City?

“Lawama zilikuwa nyingi pale yaani uwezo niliokuwa nauonyesha watu hawajali sasa mimi siwezi kufanya kazi kwenye mazingira hayo.

“Nayakumbuka maisha ya Mbeya City niliyapitia msimu wa mwisho nikiwa Simba ambapo lawama zilikuwa nyingi hasa timu inapofungwa kila mtu anakuja na kusema Kaseja kafungisha kiasi kwamba maneno hayo nilijikuta nikitamani kuachana na soka.

Upo tayari kurejea timu ya taifa?

“Kwa nini nisicheze wakati mimi ni Mtanzania! Hata nikiitwa leo nitarejea na nitacheza kwa kuonyesha uzalendo wangu, nakumbuka wakati ambao nilikuwa na msuguano na Kocha Marcio Maximo watu waliona kama ndiyo nimesusa kuichezea timu hiyo lakini mimi moyoni nilisema Maximo siyo Mtanzania na ipo siku ataondoka na kuiacha timu hiyo, yeye hatakuwa na machungu tena na sisi lakini kwangu nitaendelea kuumia endapo tukifanya vibaya kwa sababu mimi ni mzawa.

Kuhusu Mbaraka Yusuph kutokuwepo katika kuwania Tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu

“(Huyu ni straika wa Kagera Sugar) ni wazi ndiye aliyetakiwa kuwa mchezaji bora wa ligi kwa sababu ametumika ndani ya timu ambayo haina msaada mkubwa tofauti na wale ambao walipendekezwa kugombea tuzo ile.

“Angalia kama Msuva (Simon) au Niyonzima (Haruna) pale Yanga wanazungukwa na utitiri wa wachezaji ambao wana uwezo wa juu hata kwa Kichuya (Shiza) na Tshabalala (Mohammed Hussein) wote wa Simba nao ipo hivyohivyo, lakini kwa Mbaraka yeye alikuwa anapambana peke yake lakini akajituma na mwishowe akafunga mabao 12 jambo ambalo siyo jepesi hata kidogo,” anasema Kaseja.

Chapisha Maoni

0 Maoni